Kamati Tendaji ya Utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF) imekutana kwa mara kwanza katika ukumbi wa hoteli ya Morena, Morogoro, tarehe 16 Oktoba 2024, ikiwa na lengo la kupitia na kuidhinisha nyaraka muhimu za kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi huo nchini Tanzania.
Wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang'a aliwashukuru wajumbe wa kamati tendaji kwa kukubali kuwa sehemu ya kusimamia utekelezaji wa Mradi wa SOFF Tanzania.
Aidha, Dkt. Chang’a alitoa shukrani zake za dhati kwa Sekretarieti ya SOFF na WMO kwa kuichagua Tanzania kuwa miongoni mwa wanufaika wa ufadhili wa fedha za Mfuko huo takribani dola za kimarekani milioni 9.
"Uwepo wenu ni ushahidi tosha wa dhamira yenu ya kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa kwa nchi yetu, kikanda na Duniani kote, huduma ambazo zitaenda kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi”, alisema Dkt. Chang'a.
Aidha, Dkt. Chang'a aliongeza kuwa uanzishwaji wa mradi wa SOFF utasidia nchi kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa data za hali ya hewa na mfumo wa mawasiliano wa ubadilishanaji wa data hizo kimataifa kwa kuwezesha masuala ya muhimu ya kiufundi na kifedha.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Ndg. Shigeki Komatsubara alieleza jinsi anavyoridhishwa na uongozi mzuri na utendaji kazi wa TMA na wataalamu wake kwa ujumla, na kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika bara la Afrika.
Aidha, alisisitiza kuwa mradi wa SOFF utatoa msaada endelevu wa uendeshaji na matengenezo na usimamizi kwa vituo vya hali ya hewa vitakavyojengwa kuwa katika hali nzuri na endelevu kwa muda mrefu kwa kuwa UNDP imejipanga kikamilifu katika kufikia malengo na mafanikio hayo.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Bi Clara Makenya aliendelea kusisitiza umuhimu mkubwa wa kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na kuimarisha huduma za hali ya hewa.
Bi Clara pia alifafanua jukumu la UNEP katika kufanikisha mradi huo, ikiwa ni pamoja na kusimamia viwango vya ubora katika utekelezaji wa mradi hususan eneo la mazingira kwa kuratibu na kutoa ushauri pale inapobidi kwa maendeleo endelevu ya nchi na dunia kwa ujumla.
Post A Comment: