Taasisi ya World Travel Awards imetangaza hifadhi mbili za Tanzania kuwa washindi katika vipengele vya hifadhi na kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024.
Hifadhi ya Taifa Serengeti imetangazwa kuwa mshindi katika kipengele cha Hifadhi Bora Barani Afrika (“Africa’s Leading National Park 2024”) wakati Mlima Kilimanjaro ikitangazwa kuwa Kivutio bora cha Utalii Barani Afrika (African Leading Tourist Attraction 2024).
Tuzo hizo zimetolewa usiku wa tarehe 18 Oktoba, 2024 katika Ukumbi wa Hotel ya Diamonds Leisure Beach & Golf Resort ya nchini Kenya.
Akitangaza washindi, Mwanzilishi wa Taasisi ya World Travel Awards, Bwana Graham Cooke alisema kuwa Serengeti imezishinda hifadhi zingine kwa ubora barani Afrika ambazo ni Maasai Mara ya nchini Kenya, Kruger ya Afrika Kusini, Central Kalahari ya Botswana, Etosha ya Namibia na Kidepo Valley ya nchini Uganda.
Bwana Cooke alisema kuwa Mlima Kilimanjaro pia umevishinda vivutio vingine vya utalii barani Afrika ambavyo ni hifadhi ya Ngorongoro, Hartbeespoort aerial cableway, V& A Waterfront, Robben Island, Table Mountain ya Afrika Kusini, zote za Afrika Kusini, Ziwa Malawi, Okavango Delta ya Botswana, na Pyramid of Giza ya Misri.
Tuzo hizo zimepokelewa na ujumbe wa unaongozwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Bw. Ephraim Mafuru, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini CPA. Hadija Ramadhani, Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrita Lyimo pamoja na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Stephano Msumi.
Ushindi huu wa Kishindo wa Serengeti ikiwa ni mshindi wa tuzo ya Hifadhi Bora barani Afrika ni wa mara ya sita mfululizo kuanzia mwaka 2019 hadi sasa 2024. Ushindi wa mwaka huu pamoja na jitihada zingine, umechagizwa na kampeni ya TANAPA ya ‘Vote Now’ iliyofanyika kwa miezi mitatu mfululizo.
Kwa upande wa Mlima Kilimanjaro umeshinda tuzo ya kivutio Bora Barani Afrika mwaka 2013, 2015, 2016, 2017, 2018, na sasa 2024 ikiwa ni mara ya sita.
Post A Comment: