Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) amejiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Kituo cha Ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Misigiri kilichopo Kata ya Ulemo wilayani Iramba, mkoani Singida.

Baada ya zoezi hilo Dkt. Nchemba amezungumza na wananchi kadhaa wa eneo hilo waliojitokeza kujiandikisha na kuwaelimisha umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo la uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Akizungumza na wananchi hao ametoa rai kwa wananchi kutambua kuwa uandikishaji wa daftari la kudumu la uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Septemba mwaka huu, haumpi sifa mwananchi kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa isipokuwa hadi ajiandikishe kwenye daftari litakalomwezesha kuwachagua viongozi anaowataka katika ngazi ya Serikali za Mitaa.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari la uchaguzi wa Serikali za Mitaa lililozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Oktoba mwaka huu hadi tarehe 20 Oktoba ili kumchagua kiongozi atakayeungana na Serikali kuwaletea maendeleo.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi kuwa mjitokeze kujiandikisha kwani zoezi halitumii muda mrefu, ndani ya dakika moja unakuwa umemaliza kujiandikisha,” amesema Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba aliambatana na Mkewe Bi. Neema Ngure katika zoezi hilo ambalo linalenga kuandikisha wananchi 141,000 katika Wilaya hiyo.

Share To:

Post A Comment: