Na Benny Mwaipaja, Washington D.C


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amezihimiza nchi za Afrika kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha Duniani pamoja na Sekta Binafsi,  kuhakikisha kuwa zinawekeza kwenye uzalishaji wa nishati ya uhakika na yenye gharama nafuu ili kutimiza malengo ya kujiimarisha kiuchumi, kuchochea uwekezaji,  uzalishaji wa bidhaa na huduma na kukuza ajira.

Dkt. Nchemba ameyasema hayo Jijini Washington D.C, nchini Marekani, wakati akishiriki mjadala kuhusu kuiwezesha Afrika kuwa na nishati ya uhakika, ulioandaliwa na Taasisi ya Mission 300, Kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF na Benki ya Dunia.

Dkt. Nchemba amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa makundi mbalimbali katika kuzalisha nishati ikiwemo sekta binafsi, utachochea maendeleo katika Bara la Afrika kwa kuzalisha umeme wa kutosha na pia kufanyabiashara ya kuuziana umeme.

Alisema kuwa Tanzania kwa upande wake, kwa kushirikiana na mradi wa Benki ya Dunia wa kusaidia upatikanaji wa umeme wenye thamani yad ola za Marekani milioni 300, vijiji 11,837 vimeunganishwa na umeme na kuchochea maendeleo ya watu katika maeneo ya vijijini.

Aidha, alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme nchini, unakwenda sambamba na hamasa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuweka sera, mipango, mikakati na kanuni zitakazochochea matumizi ya nishati hiyo safi ya kupikia.

Dkt. Nchemba alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau wa maendeleo na Mawaziri wa Fedha wa nchi za Afrika kuwashawishi Wakuu wa nchi zao kushiriki Kilele cha Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu Nishati unaotarajiwa kufanyika Jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa mwezi januari mwaka 2025. 

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB anayesimamia masuala ya Nishati, Dkt. Kevin Kariuki, amesema kuwa Taasisi ya Mission 300 inajukumu la kuhakikisha kuwa suala la nishati linapewa kipaumbele katika mipango na sera za nchi za Afrika kutokana na umuhiku wake katika kukuza uchumi, usalama na kuharakisha maendeleo ya watu.

Alifafanua kuwa Mkutano wa Kilele wa Nishati utakaowashirikisha Wakuu wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara utakaofanyika Jijini Dar es Salaam nchini Tanzania kuanzia tarehe 27 hadi 29 mwezi Januari mwaka 2025, utaweka mikakati na uwezeshaji kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme.

Inakadiriwa kuwa Watu zaidi ya milioni 300 wanatarajiwa kuwa watakuwa wameunganishwa na umeme katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ifikapo Mwaka 2030, ikiwa ni jitihada za pamoja za wadau zikiwemo Taasisi za Fedha za Kimataifa na Sekta Binafsi kufanikisha mradi huo






.
Share To:

Post A Comment: