Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo mkoani Rukwa, kutokana na uwepo wa Madini ya Ulanga, Shaba, Emerald, Titanium, Dhahabu, Hellium, Makaa ya Mawe na Aquamarine ili kuvutia wawekezaji na kuongeza tija katika uchumi wa mkoa huo. 

Amesema hayo leo Oktoba 23, 2024, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo ambako amesisitiza kwamba lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha kuwa rasilimali za madini zilizopo nchini, ikiwemo mkoa wa Rukwa, zinawanufaisha Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza na Wachimbaji Wadogo wa Madini baada ya kukagua shuguli za uchimbaji mdogo katika Kijiji cha Mponda, Manispaa ya Sumbawanga, Dkt. Kiruswa ameeleza kuwa serikali haitaki kuona wachimbaji wadogo wakichimba kwa kubahatisha katika shughuli zao hivyo kupitia Mpango wa Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri Serikali imepanga kuongeza utafiti wa kijiolojia nchini ili kusaidia kuboresha kanzidata ya hifadhi ya madini tulinayo hapa nchini.

“Ndugu zangu, kiwango cha utafiti wa kina wa kijiolojia kwa Tanzania nzima ni asilimia 16 tu, lakini serikali inalenga kufikia angalau asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo na wawekezaji wakiwemo wa Rukwa wanakuwa na taarifa za kina za kijiolojia ili kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza katika uchimbaji wa madini kwa kufanya shughuli zao kwa uhakika” amesema Dkt. Kiruswa

Pamoja na hayo, Dkt. Kiruswa amebainisha kwamba Serikali kupitia Shirika la Taifa la Madini (STAMICO) itaendelea kutoa msaada wa vifaa vya kisasa kwa wachimbaji wadogo, ikiwa ni pamoja na mashine za uchorongaji na kwamba vifaa hivyo vya kisasa vitawawezesha wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, kuboresha uzalishaji, na kuongeza thamani ya madini yanayopatikana

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, ameeleza kuwa Ofisi ya Madini ya mkoa huo imefanya ukaguzi na tathmini ya kina ya maeneo mbalimbali yanayofaa kwa shughuli za uchimbaji wa madini, hususan kwa wachimbaji wadogo. 

Kulingana na Mhandisi Kumburu, tathmini hiyo imelenga kubaini maeneo yenye rasilimali za madini ili kutoa fursa kwa wachimbaji wadogo kuomba leseni na kuanza shughuli za uchimbaji na kueleza kuwa hatua hiyo inalenga kurahisisha upatikanaji wa leseni, kuvutia wawekezaji wapya, na kuongeza mapato ya serikali kupitia sekta ya madini na kuwa timu ya ukaguzi ilitembelea jumla ya maeneo 13, na kwamba maeneo hayo yamependekezwa kutengwa kwa utaratibu maalum kwa wachimbaji wadogo. Maeneo haya yamebainika kuwa na viashiria vya madini na hivyo yana uwezo wa kuzalisha madini kwa kiwango cha kuridhisha.

“Tathmini ya awali iliyofanywa katika maeneo hayo imethibitisha uwepo wa madini katika eneo lenye ukubwa wa hekari 7,180, ambalo lina uwezo wa kutoa leseni ndogo 718 kwa wachimbaji wadogo. Hii itatoa fursa zaidi kwa wachimbaji hao kuingia rasmi katika sekta ya madini kwa utaratibu ulio rasmi na ulio rahisi lakini pia tayari wawekezaji wapya 10 wamejitokeza na kuonyesha nia ya kuwekeza katika fursa za uchimbaji wa madini zilizopo mkoani Rukwa” amesema Mhandisi Kumburu.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Nyakia Chirukile amesema kuwa uwepo wa rasilimali madini katika mkoa huo kwa wingi kutasaidia kuufungua mkoa huo kibiashara kwani kwa miaka mingi wamekuwa wakitegemea Zaidi mazao ya chakula lakini ikiwa uwekezaji wa madini utaongezeka katika mkoa wa Rukwa ni matumaini yao kuwa mkoa utaingia katik ramani ya shughuli za uzalishaji madini na kufunguka Zaidi kiuchumi.











Share To:

Post A Comment: