Mkuu wa wilaya ya ilala Edward Mpogolo ameanza ziara ya kata kwa kata katika makazi ya wananchi na vijiwe vya bodaboda, bajaji na masoko kuwaelimisha umuhimu wa kujiandikisha na kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa utaofanyika novemba 27 nchini.
Mpogolo ameanza ziara yake ya kuhamasisha katika makutano ya barabara mataa ya kamata kata ya gerezani kuelimisha shirikisho la vyama vya bodaboda na bajaji pamoja na wasafiri wengine wa vyombo vya moto.
Akizungumza na wananchi, makundi mbalimbali ya kijamii Mpogolo amewataka wananchi na makundi yote kujitokeza kujiandikisha kwa siku nne zilizosalia na kujitokeza kupiga kura.
Amesema ni muhimu kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa kwa wananchi wote wenye sifa kuanzia miaka 18 na kuendelea, mkazi halali wa mtaa huo, mwenye akili timamu ana haki ya kujiandikisha na kupiga kura katika zoezi lililoanza tarehe 11 hadi 20 na uchaguzi ni tarehe 27 mwezi ujao.
Ameeleza kuwa umuhimu wa zoezi ili ni mkubwa kwa wananchi wote wenye sifa kujua uchaguzi wa mitaa unawahusu kuchagua viongozi wao wa mitaa wanaokua nao katika makazi yao na kusaidia kutatua kero zao za kijamii.
Amebainisha asili ya uchaguzi wa mitaa ni kutokana na serikali kuu kugatua madaraka kushusha katika ngazi za mitaa, vijiji na vitongoji ili wananchi wafanye maamuzi yao.
Akiongea na wananchi wa kata ya vingunguti , banana ,kitunda, kitunda shule , kivule sokoni , fremu kumi, msongola, chanika, zingiziwa na gongo la mboto Mpogolo amesema wilaya ya ilala ina vituo 454 katika mitaa 159 ambavyo vinafunguliwa na kufungwa kwa wakati.
Mpogolo amesema ushiriki wa wananchi katika uchaguzi utawasaidia kupata viongozi bora, wanaosoma mapato na matumizi, wanaofanya mikutano na kusimamia ulinzi na usalama katika mitaa yao.
Kuhusu baadhi ya watu wanaowazua wananchi wenye sifa za kujiandika kwenda vituoni Mpogolo ameliagiza jeshi la polisi Mkoa wa ilala kufanya msako wa kuwakamata na kuwafikisha mahakakamani ndani ya siku mbili.
Aidha Mpogolo ametumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi, halmashauri ya jiji ina zaidi ya bilioni 11 kuwakopesha makundi ya bodaboda na bajaji au mmoja mmoja kupata mikopo ya almashauri ambayo inatolewa kwa kundi la wanawake, vijana na walemavu.
Mikopo ambayo kwa sasa imeongezwa sifa kutoka umri wa miaka 35 hadi 45 tofauti na mikopo ya awali ilivyokua.
Akizungumzia suala la barabara ya Kitunda, kivule hadi msongola amewahakikishia wananchi, wafanyabiashara, bodaboda na bajaji barabara hiyo imeshapata mkandarasi na mkataba wa ujenzi huo utashuhudiwa na Waziri wa nchi ofisi ya Rais tawala za serikali za mikoa na mitaa Tamisemi Mohamedy Mchengerwa wakati wowote kuanzia sasa.
Barabara ambayo itajengwa katika kiwango cha lami, mifereji, taa za barabarani na kuwa katika viwango vya kisasa ili kumaliza changamoto ya muda mrefu kwa wakazi wa kata ya kitunda, kivule na msongola.
Mpogolo amesema maendeleo ya wananchi katika sekta ya elimu, afya, miundombinu, na maji yanaanzia serikali za mitaa.
Kwa upande wa jeshi la polisi kupitia kwa mrakibu wake SP Kasira kwa niaba ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es salaam amewahakikishia wananchi jeshi la polisi liko makini kuhakikisha ulinzi na usalama wakati wa kipindi cha kujiandikisha na kupiga kura unakuwa wa kutosha.
Nae Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya bodaboda na bajaji Hussein Chanje ameishukuru Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia kwa kuwasaidia maafisa usafirishaji kutambulika rasmi, kuingia mjini na kuongeza umri wa kuchukua mikopo kutoka miaka 35 hadi 45 hali inayofanya wafanye kazi zao kwa amani.
Umoja huo kupitia Mwenyekiti wao wamehakikisha kushiriki vilivyo kujiandikisha na kupiga kura pamoja na kuhamasisha makundi mengine.
Huu ni mwendelezo wa Mkuu wa wilaya ya ilala Edward Mpogolo kuhamasisha zoezi la kujiandikisha na kupiga kura ambalo alilianzia mapema katika kata zote 36 za ilala, vijiwe vya kahawa, magazeti, michezo na kuendelea katika masoko, vijiwe vya bajaji, bodaboda, babalishe na mamalishe.
Post A Comment: