Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekagua na kuridhishwa na ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya Utete, Rufiji inayogharimu Shilingi Milioni 900 ikiwa ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuboresha utoaji wa huduma bora za Afya kwa wananchi.

Bashungwa amefanya ukaguzi huo Oktoba 24, 2024 Mkoani Pwani na kueleza kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini ambapo ameiboresha hospitali ya wilaya Utete iliyojengwa tangu mwaka 1967 kuwa ya kisasa.

“Wananchi mnaishi Rufiji mnajua hospitali hii ilijengwa mwaka 1967 ilikuwa ina muonekano wa kizamani lakini kwa kazi kubwa anayoifanya Rais Dkt. Samia ameleta fedha hapa ili hospitali hii ifanyiwe ukarabati mkubwa na hakika ukiangalia majengo yalivyokuwa na sasa hivi, yamekamilka kwa kweli Rufiji sio ile ya zamani”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameipongeza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji kwa kuendelea kusimamia vizuri fedha zinazoletwa na Serikali katika miradi ya maendeleo hususan Sekta ya Afya.

Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Dkt. Hamis Abdallah ameeleza kuwa ukarabati wa miundombinu katika hospitali  hiyo umefikia asilimia 85 na unatekelezwa na kampuni ya uhandisi ya AMAR Builders ukihusisha ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la upasuaji, jengo maabara, jengo la wodi ya wanawake, jengo la CTC, jengo la TB, jengo la RCH, jengo la maternity pamoja na Korido.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amemshukuru Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 900 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya Hospitali ya Wilaya ya Utete.








Share To:

Post A Comment: