JUMUIYA ya Wanyapori ya Enduimet(WMA) Wilayani Longido Mkoani Arusha imechangia shilingi milioni 22 na vitanda 10 kwaajili ya mabweni mawili ya wasichana ya shule ya sekondari ya Enduimet iliyopo Wilayani Longido Mkoani Arusha yaliyoungua moto mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu.

Shule ya sekondari ya Enduiment iliyopo Kijiji cha Lerangwa Kata ya Olmology Tarafa ya Enduiment Longido mabweni mawili yaliungua moto usiku wa agosti 26 mwaka huu na chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

Akizungumza na Walimu na wanafunzi wa shule ya sekondari Enduimet,Makamu Mwenyekiti wa WMA, Peter Lekanet ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido alisema kiasi hicho cha pesa ni kufuatia michango ya shilingi milioni 2 kwa vijiji 11 vya Tarafa ya Enduimet.

Lekanet alisema pamoja na mchango huo wa fedha utakaosaidia ununuzi wa vitanda,magodoro na blanket pia vijiji hivyo vimetoa msaada wa vitanda 10 kwa shule hiyo kwa ajili ya wanafunzi ambao bado wanauhitaji Kwa sababu wanafunzi bado wanalala chini baada ya vitanda vya awali,magodoro na blanket vyote kuungua moto.

Makamu Mwenyekiti wa WMA na Halmashauri ya Longido aliwaomba wadau mbalimbali wa elimu na Maendeleo Longido kujitoa katika kuwasaidia wanafunzi hao kwani mahitaji ya wanafunzi ni makubwa na kumwachia Mbunge wa Jimbo la Longido na Naibu Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa pekee yake sio sawa kwani wanafunzi wanaosoma shule hiyo ni wa ndani ya Longido na nje ya Longido.

Naye Mke wa Kiruswa,Agnes Kiruswa akikabidhi magodoro 80 na Blanket 100 na vichujia maji 8 maji Kwa niaba ya Mbunge alisema malengo ya Mbunge bado hayajatimia hivyo amekabidhi kiasi ili kutimiza malengo ya magodoro 485 na Blanket za kiasi hicho kwa mabweni mawili ya wasichana  ya shule hiyo.

Alisema Mbunge kama alivyoahidi atafanya hivyo ila wasichana nao wanapaswa kusoma na kufanya vema katika mitihani ya Kitaifa ili wwweze kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuacha mara moja mambo yasiyokuwa ya msingi kwani yanaweza kurudisha nyuma malengo yaliyokusudiwa.

Makamu Mkuu wa shule ya Enduimet. Mwalimu Williamu Mangochi alimshukuru Sana Mbunge Kiruswa Kwa Moyo wa kujitoa na kumwomba kuendelea na Moyo huo Kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo waliopata majanga kwani kufanya hivyo kunawapa moyo wanafunzi hao Kwa kuona viongozi wanawajali na wanajitoa kuwasaidia.

Mwalimu Mangochi aliwaomba wadau wengine kuiga mfano wa Mbunge kwani shule hiyo sio ya Mbunge pekee yake bali ni ya wazazi wa Longido na nje ya Longido hivyo wadau wote wa Maendeleo Longido wanapaswa kujitoa kwa hali na mali kuwasaidia wanafunzi hao kulala sehemu Salama.

Naye Rais wa Wanafunzi,Flora Shirima alimshukuru Mbunge Kiruswa kwa msaada huo na kusema kuwa Mbunge huyo ana moyo wa kusaidia hivyo Mwenyezi Mungu atamlipa Kwa kila Jambo jema analofanya Kwa shule hiyo na Longido kwa ujumla.

Shule hiyo inahitajika kujengwa mabweni matatu kwa gharama shilingi milioni 390,vitanda 170 vinapaswa kununuwa kwa gharama ya shilingi milioni 142 na magodoro 340 yanapaswa kununuliwa kwa gharama ya shilingi milioni milioni 60.

Mabweni yaliungua moto wakati wanafunzi wanapata mlo wa jioni na baadae waende darasani kwa masomo ya jioni na ndani ya bweni kulikuwa na mwanafunzi mmoja aliyekuwa mgonjwa na walipofanya uhakiki mwanafunzi huyo alikuwa ametoka nje wakati moto ukiwaka.



Share To:

Post A Comment: