Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WIZARA ya fedha imetoa rai kwa Watanzania hususan makundi ya akinamama na wajasiriamali kujiepusha na mikopo ya udhalilishaji isiyo rasmi na badala yake watumie Taasisi zilizosajiliwa na kutambulika ili kulinda fedha zao.


Aidha imekemea Taasisi zinazotoa huduma za mikopo ambazo hazijasajiliwa kufuata sheria za usajili na kupata leseni ili kuondoa migongano isiyo ya Lazima.


Akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Kibaha, katika ukumbi mkubwa wa mikutano Halmashauri ya Kibaha septemba 11,2024 ,Ofisa Usimamizi wa fedha kutoka Wizara ya Fedha Stanley Kibakaya alieleza utoaji elimu hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alilolitoa baada ya baadhi ya wananchi kulalamikia watoa huduma kutoa riba kubwa.


"Utekelezaji huu ni agizo la Rais wetu ambalo aliagiza Wizara ya Fedha kupita kwa watanzania kutoa elimu ya fedha,mikopo rafiki isiyo ya udhalilishaji na kueleza umuhimu kutumia Taasisi zinazotambulika kisheria zilizosajiliwa ikiwemo UTT-Amis,Benki na Sacco's."alifafanua Kibakaya.


Alieleza utekelezaji wa mpango huo ni wa miaka kumi (10)ambapo utakamilika 2030 na hadi sasa wameshatoa elimu katika mikoa 13 ikiwa ni pamoja na Pwani na Morogoro.


"Kipengele cha pili ni Wizara ya Fedha kushirikiana na Taasisi za kifedha kufikia watanzania ambapo lengo ni kufikia watanzania asilimia 80 ifikapo 2025" aliongeza kusema Kibakaya.


Ramadhani Myonga Ofisa Sheria Mwandamizi na Mtatuzi wa malalamiko ya wateja wa Taasisi za fedha (Benki Kuu ya Tanzania) aliwataka wananchi kuwa na usimamizi mzuri wa fedha Binafsi ili fedha wanayopata iongeze thamani.


Vilevile aliwaasa kujenga tabia na tamaduni ya kuwa na vyanzo vya mapato vilivyoendelevu .


"Oya ,Kausha Damu sio mikopo rasmi kupitia elimu hii leo badilikeni mkawe mabalozi kutambua Taasisi zilizosajiliwa na kwenda kujiunga nazo kwa ajili ya usalama wa fedha zenu"alieleza Myonga.


Awali Ofisa Masoko na Uhusiano Mwandamizi kutoka UTT-AMIS, Rahim Mwanga, alitoa rai kwa washiriki kuwa na tabia ya kuweka akiba kwa faida yao badala ya kutumia kwa matumizi yasiyo sahihi.



Aliwataka wanapokopa watunze kumbukumbu na kufuatilia mikataba kwa Taasisi zinazotoa huduma za mikopo.


Mkazi wa Sofu Anna Mwakihaba ,aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwapa elimu hiyo kwani awali walikuwa hawana uelewa wa masuala ya fedha na mikopo.
Share To:

Post A Comment: