Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb), amewataka viongozi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutumia vyombo vya habari ili kutangaza shughuli mbalimbali zinazofanywa na mfuko huo.

Mhandisi Mahundi amesema hayo tarehe 10 Septemba, 2024, wakati wa ziara yake katika ofisi za UCSAF Kanda ya Pwani zilizopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ambapo alikagua shughuli mbalimbali pamoja na mradi wa Tanzania ya Kidijitali wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini.

“Mahusiano na vyombo vyetu vya habari ni muhimu, Ukifanya kazi ukikaa nayo, hakuna atakayejua umefanya hivyo. Ni muhimu kuvishirikisha katika utekelezaji wa shughuli zenu mbalimbali,” amesisitiza Mhandisi Mahundi.

Aidha, Naibu Waziri huyo amehimiza UCSAF kuwashirikisha viongozi mbalimbali, wakiwemo wabunge, wanapotoa huduma za mawasiliano katika maeneo yao.
Amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia katika kupata taarifa sahihi za maendeleo katika maeneo husika.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mahundi amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano vijijini, akieleza kuwa kumekuwa na mahitaji makubwa ya mawasiliano katika maeneo mengi.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema tayari wameshakaa kikao na kampuni za simu na kuweka utaratibu mzuri wa kukamilisha ujenzi wa minara hiyo, pamoja na kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli zinazofanywa na mfuko huo.
Share To:

Post A Comment: