Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewataka watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma, kuendelea kushiriki masuala ya kijamii ili kujenga mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka.

Mhe. Simbachawene ametoa maelelekezo hayo jijini Dodoma katika siku ya tume ambayo maadhimisho yake yameenda sambamba na kufanyika kwa matendo ya huruma kwa watu wenye uhitaji pamoja na upandaji wa miti katika jengo la Tume ya Utumishi wa Umma lililopo katika mji wa serikali Mtumba. 

“Mmefanya jambo jema kumpatia bajaji mwenzetu mwenye mahitaji maalumu na mmeahidi kumuwekea mafuta, pia mmesema mnaenda Hombolo kutoa msaada kwa wenye uhitaji katika kituo cha wazee wa Samaria” Mhe. Simbachawene ameeleza.

Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa, kitendo cha Tume ya Utumishi wa Umma kufanya hayo yote ni ishara ya upendo na ni matendo yanayompendeza Mungu na kumfariji mwanadamu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Jaji mst. Hamisa Kalombola, wakati akikabidhi vyoo vilivyojengwa kwa ajili ya wenye uhitaji katika kijiji cha Samaria amewasihi wanufaika kuvitunza na kuzingatia usafi ili vidumu.

“Kuna methali inasema, vitunze vidumu kwahiyo maana yake hata mkiwa na vyoo mia mbili lakini msipovitunza havitadumu” Jaji mst. Kalombola amesisitiza.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wanufaika wenzie, mzee Antony Cyprian ameushukuru uongozi na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma kwa kuwapatia msaada wa kuwajengea vyoo, ambavyo vimetatua changamoto waliyokuwa wakikabilina nayo.

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma, Afisa Tawala Mwandamizi Bi. Dina Moshi amesema ushirikiano waliokuwanao umewawezesha kutoa msaada wa vyakula, vifaa vya usafi pamoja na mavazi wenye samani ya zaidi ya shilingi milioni tatu na kuongeza kuwa kiasi cha zaidi ya milioni 13 kimetumika kujenga vyoo nane.

Tume ya Utumishi wa Umma imeadhimisha siku ya tume kwa kupanda miti na kufanya matendo ya huruma, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Share To:

Post A Comment: