Na. Saidina Msangi, Kibaha, Pwani.


Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau na Taasisi zilizo chini yake imejipanga kutoa elimu ya fedha kwa Watanzania asilimia 80 ifikapo mwaka 2025 ili wawezesha wananchi kufahamu umuhimu wa akiba, bima, usimamizi wa fedha binafsi pamoja na kutumia watoa huduma rasmi wa fedha waliosajiliwa.

Hayo yamebainishwa na Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha m, Bw. Stanley Kibakaya, wakati wa kuhitimisha programu ya utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Halmashauri ya Mji Kibaha, Pwani.

Alisema kuwa elimu hiyo ya fedha imepokelewa vizuri na wananchi katika mikoa ya Kagera, Manyara, Singida, Kigoma, Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Mtwara, Morogoro, Lindi na mikoa mingine inatarajiwa kufikiwa katika awamu ijayo. 

‘‘Tunafanyia kazi maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa Wizara ya Fedha kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi na pia mpango wa sekta ya fedha unalenga kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia taasisi za fedha zilizosajiliwa wanapochukua mikopo ili kuwawezesha kuondokana na mikopo umiza,’’alisema Bw. Kibakaya.

Alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa elimu ya fedha na wananchi wameifurahia na kukiri kuwa elimu hiyo imewasaidia na wataenda kuzitumia huduma rasmi za fedha ikiwemo kuweka akiba, uwekezaji na bima.

Kwa upande wao wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Pwani, wameipongeza Serikali kwa kuwapatia elimu hiyo muhimu ambayo wanaeleza kuwa itawawezesha kujikwamua kiuchumi pamoja na kujiandaa kutumia fursa za uwekezaji katika mifumo rasmi ikiwemo UTT AMIS.
Share To:

Post A Comment: