Wanawake kutoka jamii ya kimaasai katika Tarafa ya Longido wilaya ya Longido mkoa wa Arusha wameonyesha furaha yao baada ya shirika la Legal Services Facility (LSF) kuwajengea uwezo wa kutambua haki zao.
Shirika hilo limewawezesha wanawake hao Kwa kuwapatia elimu ya haki za binadamu, haki ya kushiriki katika siasa, afya pamoja na elimu Kwa watoto wa kike.
Akizungumza kwenye kigoda cha mwanawake katika wiki ya AZAKI wilayani humo, Mkurugenzi wa LSF Lulu Mwakilala amesema shirika hilo linahakikisha kuwa watu wote wanapata haki sawa hasa wanawake na watoto wa kike.
"LSF tunashirikiana na serikali kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya juu ili kuhakikisha kuwakuwepo na usawa kati ya mwanamke na mwanaume katika jamii" amesema Mwakilala.
Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Longido Upendo Ndorosi amesema kwa sasa kuna mwitikio wa wanawake kushiriki kwenye siasa tofauti na hapo nyuma wakati anagombe nafasi aliyonayo.
Anasema changamoto hiyo ilitokana na mfumo dume uliokuwepo ambao shirika la LSF limesaidia kutoa elimu ambayo imeondoa dhana hiyo na sasa hali inaridhisha kidogo.
"Elimu inayotolewa na mashirika ya kiraia yamewasaidia sana wanawake kupata ujasiri ambapo mpaka sasa katika wilaya hii kuna wanawake kumi na moja ambao nimewashawishi ili wagombee kwenye uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu" amesema Ndorosi.
Nabore Nabak ambaye ni Mwenyekiti wa vikundi zaidi ya 300 vya maendeleo wilaya ya Longido amesema wanawake katika wilaya hiyo wanapitia changamoto kadhaa katika harakati za kutafuta usawa.
"Lakini kupitia vikundi hivi inaonyesha kuwa mwanamke wameelimika na wameionyesha jamii kuwa wanaweza wakaongoza huku akitimiza majukumu yake ya nyumbani" amesema Nabak.
Hata hivyo kwa upande wake kiongozi wa mila Laigwanani Lucas Sambeke amesema kwa sasa kupitia vikao vyao vya mila wamekuwa na agenda ya kumuinua mwanamke na mtoto wa kike baada ya kuona matokeo chanya kutoka kwa wanawake.
"Mila zetu zilikuwa zinamkandamiza mwanamke, lakini tumefanikiwa kwa
Asilimia kubwa kushawishi wazee wengine wa mila kupitia sherehe na vikao Ili kuruhusu mwanamke aweze kufanya shughuli za uongozi" amesema Laigwanani Sambeke.
Post A Comment: