Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii yaahidi kuendelea kuimarisha juhudi za mazingira za kikanda na kukuza suluhu za pamoja kwa mabadiliko ya hali ya hewa na uhifadhi wa utofauti wa kibaiolojia katika Bonde la Congo.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt Pindi Chana katika Mkutano uliohusisha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC) pamoja na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo (CBFF) jijini Dodoma.

Amesema Mkutano huo umejikita katika kuimarisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kuongeza ushirikiano kati ya pande hizi tatu katika juhudi za kulinda mazingira na kuendeleza uhifadhi.

“Tanzania, kama mwanachama wa CBCC, tunakwenda kunufaika na utaratibu wa pamoja wa usimamizi wa rasilimali za maliasili, rasilimali fedha, na kuimarisha mifumo ikolojia ya eneo letu kupitia Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo pamoja na Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) katika kutekeleza makubaliano ya utunzaji Mazingira ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Paris na malengo ya maendeleo endelevu,”

Aidha ongezeko la watu duniani nchi wanachama zimeona kuna umuhimu wa kuungana na kuwa na sauti ya pamoja katika majadiliano ya kimataifa kuhusu usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, huku zikichangia uzoefu wao na kupokea maarifa mapya kutoka kwa nchi nyingine wanachama utakaosaidia uboreshwaji wa sera.
kupitia mkutano huo mambo kadhaa yamezungumzwa ikiwemo namna gani nchi wanachama zinaweza kuendeleza Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo lakini pia kuongeza uwezo wa wataalamu katika kulinda mazingira na maboresho ya sera ili mazingira yasiharibiwe.


Kwa upande wake Waziri wa Utalii na Mazingira wa Jamhuri ya Kongo na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo (CBCC), Mhe. Arlette Soudan – Nonault alisema pamoja na mambo mengine wamefanikiwa kukubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kujua namna gani wanaweza kuzisaidia nchi wanachama kupata fedha ambazo tayari zimewekwa katika mfuko wa blue na benki mbalimbali wanazofanya nazo kazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utalii na mabadiliko ya tabianchi.


“kamisheni hiyo imeahidi kushirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali ili kufanikisha dhamira ya kamisheni hiyo na katika kuhakikisha hilo mwakani kutakuwa na mkutano mkubwa wa wakuu wa nchi kwa ajili ya kusaidia kamisheni hiyo kufanya kazi huku akisisitiza kuanzisha kwa redio na luninga itakayofanya kazi kwa lugha nne ambapo nchi wanachama zitashiriki kutoa maudhui.” Alisema, Soudan – Nonault.


Naye Jean Paterne MEGNE EKOGA, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) na Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Utawala wa kamisheni hiyo anasema wao jukumu lao kubwa ni kuratibu upatikanaji wa fedha zitakazozisaidia nchi wanachama na mashirika yasio ya kiserikali kuisaidia kamisheni hiyo kufikia malengo yake.


Naye Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na mwakilishi wa nchi katika mfuko wa Blue wa Bonde la Congo, Prof. Dos Santos Silayo alisema kamisheni hiyo ilianzishwa na inaundwa na nchi ambazo kijiografia, kiikolojia pamoja na kiuchumi zina uhusiano mkubwa katika kulinda na kuhifadhi bionuai na misitu ya bonde na mito ya Congo, ambayo ina umuhimu mkubwa katika ustamilivu wa bonde la Congo.

Ikumbukwe kwamba Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo unajumuisha nchi wanachama 16 ambazo zinapata fursa mbalimbali ikiwemo kuandika miradi na kuomba mashirikiano katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa hasa katika kipindi hiki ambapo kumekuwa na ongezeko kubwa la watu duniani.




Share To:

Post A Comment: