Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa ameeleza kuhusu dhamira ya Serikali ya Tanzania kuwa haifungamani na mkakati kutoka nchi moja katika kuendeleza Madini muhimu na Mkakati yanayopatikana nchini bali itashirikiana na Kampuni kutoka nchi yoyote duniani zitakazowekeza kwa kufuata misingi ya Sheria zinazosimamia Sekta ya Madini nchini 

Dkt. Kiruswa aliyasema hayo Septemba 23, 2024 jijini Las Vegas-Nevada Marekani wakati akishiriki kwenye  mjadala wa madini umuhimu na mkakati katika uchumi wa madini kwenye maonesho ya Madini (MinExpo2024) yanayoendelea nchini humo.

‘’Tanzania itashirikiana na kampuni kutoka nchi yoyote duniani ambazo zitakazowekeza nchini kwa kufuata misingi ya Sheria, za nchi zinazosimamia Sekta ya Madini,’’ alisisitiza Dkt. Kiruswa.

Aidha, aliongeza kwamba, mkakati wa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Hassan  ni kuhakikisha madini yanayozalishwa nchini ikiwemo madini muhimu na mkakati yanaongezwa thamani hapa nchini ili kuinufaisha nchi kutokana na uwepo wa rasilimali hizo ambazo taifa limebarikiwa kuwa nazo, na kuongeza‘’ Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini  na mazingira mazuri ya kulinda mitaji ya wawekezaji,’’.

Dkt. Kiruswa alieleza kuhusu miradi mbalimbali ya madini mkakati inayoendelea nchini na kueleza kuwa hadi sasa kuna miradi 12 ambayo iko tayari kwa ajili ya kuendelezwa kuwa migodi  huku sita ikihusisha  madini ya kinywe (graphite).

Vilevile, ametumia jukwaa hilo kuelezea kuhusu mikakati ya Serikali kuendeleza madini mkakati ikiwemo kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia, na kuongeza kwamba ipo kwenye mchakato wa kuandaa  Mkakati wa Madini Muhimu ambao kwa sasa uko kwenye hatua ya mashauriano na wadau.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa alitumia jukwaa hilo kuzikaribisha kampuni za utengenezaji wa vifaa na mitambo kutoka Marekani na nchi nyingine  duniani zinazoshiriki katika maonesho hayo  kushiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini unaotarajiwa kufanyika  Novemba 19- 21, 2024 jijini Dar es Salaam katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere na kueleza kuwa, wadau mbalimbali watafahamu kwa undani kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya madini nchini.

Dkt. Kiruswa ameambatana na wataalam kutoka Tume ya Madini, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO)na wadau na kampuni mbalimbali  kutoka Tanzania zikiwemo za uchimbaji na utoaji huduma migodini.










Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: