Na Denis Chambi,  Tanga.

MKUU wa wilaya ya Tanga Japhari Kubecha amesema kuwa  Serikali kwa kushirikiana na wadau pamoja na familiya ya aliyekuwa mtunzi wa vitabu hapa nchini Sheikh Shaaban Robert watajenga maktaba ya kisasa  kutunza kumbukumbu zake pamoja na kufanya tamasha maalum kila mwaka ili kumuenzi kwa kazi nzuri ambazo alizifanya ikiwa ni pamoja na kuinadi Lugha ya Kiswahili.

Kubecha ameeleza hayo September 8,2024 mara baada ya kutembelea kaburi lake na  kushiriki dua maalum ya kumwombea pamoja na kuitembelea familiya yake iliyopo katika Kijiji cha Vibandani Kata ya Masiwani jijini Tanga ambapo amesema kuwa kama mzawa ambaye aliitangaza wilaya hiyo pamoja na Mkoa kwa ujumla kupitia kazi zake jamii haina budi kuendelea kurithishwa  na kumkumbuka kwa kazi ambazo alizifanya.

"Leo tumeshauriana na familiya  tujipange kuona namna ambavyo tunaweza kumuenzi Shaaban Robert  kikamilifu bado hatujapata nafasi nzuri ya kumuenzi kama wana Tanga kwa sababu yako mambo makubwa ameyafanga ikiwemo kutumia vipawa vyake  kutangaza na kuinadi Lugha yetu adhimu ya Kiswahili yapo mambo nimewaomba kama familiya wayaangalie na kuyaratibu na yale yanayotuhusu sisi kama Serikali tutakuwa tayari kuyafanya " alisema Kubecha.

"Nimepita kuona alipozikwa yeye na watoto wake nimeiona pia maktaba hii ambayo aliichorea wafadhili ambayo sasa ni chakavu na kwa kweli imepoteza ule ubora wake sasa tunakwenda  kukaa kama Serikali kwa kushirikiana na wadau tuone ni kwa namna gani tutakwenda kuijenga maktaba ya kisasa lakini kuweka mkakati wa kuwa na kumbukizi angalau kila mwaka tutakuwa tunafanya tamasha la kumuenzi Sheikh Shaban Robert katika eneo hili ambalo aliishi"

"Sisi kama Serikali ya wilaya ya Tanga tunaahidi  kushirikiana na familiya pamoja na wadau kuendelea kuenzi mambo yote mazuri ambayo Sheikh Shaban Robert aliyafanya na hasa kukuza Lugha ya Kiswahili unapotaja vinara wa Lugha yetu adhimu ya Kiswahili huwezi kuacha kumtaja Sheikh Shaaban Robert, Lugha yetu ameipambanua duniani na wapo watu wamekuwa ma Profesa , ma Daktari wa falsafa kupitia  kupitia vitabu vya Sheikh Shaaban Robert kwa hiyo tuna kila sababu ya kumuenzi kama Mwana Tanga kwa sababu aliitangaza wilaya yetu na Mkoa wetu kwa ujumla" alisema Mkuu huyo wa wilaya.
 
Akizungumza kwa niaba ya familiya mjukumu wa Marehemu Sheikh Shaaban Robert, Mustafa Akili  ameishukuru Serikali ya wilaya ya Tanga kwa kuja na wazo la kumuenzi  Babu yao ambaye pamoja na kuwa kielelezo cha familiya ameitambulisha kitaifa na kimataifa .

"Tunashukuru kuhusu suala la Maktaba tumeshalifikisha kwa Mkuu wa wilaya natumaini kwamba watalifanyia kazi tutakaa kama familiya na kupanga kwa kushirikiana na Serikali tuone jinsia ya kumuenzi Babu yetu"

Sheikh Shaaban Robert ambaye alizaliwa mwaka 1909  katika Kijiji cha Vibandani kata ya Masiwani halmashauri ya Jiji la Tanga alifariki mwaka 1962 kwa tatizo la upungufu wa damu mwilini . Vizazi na vizazi hususani watanzania wanaendelea kumkumbuka kupitia kazi zake za utunzi wa vitabu vya Tamthiliya na Riwaya mbalimbali zikiwemo  Kusadikika, Kufikirika , Adili na nduguze , ,Mwafrika aimba ,Almas za Afrika, Pambo la Lugha , Utu bora mkulima, Mithali na mifano ya mkulima na nyinginezo 




Share To:

Post A Comment: