Serikali imesema kuwa itaanza kuchukua hatua kwa wahudumu wa afya watakaobainika kuzembea katika usafi na kusababisha mashuka ya vitanda vya wagonjwa katika hospitali wanazohudumu kufubaa hadi kubadilisha rangi zao halisi.

Mkuu wa Wilaya ya Monduli Festo Kiswaga amesema kuwa Serikali na wadau wa Afya nchini imekuwa ikipeleka mashuka meupe kwa ajili ya kutandika katika vitanda vya kulaza wagonjwa lakini baada ya mfupi zimekuwa zikifubaa na kuwa za rangi ya kahawia kitendo kinachoakisi kusababishwa na uchafu kwa kufuliwa bila kutakata.

“Uchafu katika vituo vyetu haikubaliki, hivyo tutanzaa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wahudumu watakaobainika kuzembea katika hili akiwemo mkuu wa Kituo, kama tunavyofanya mnazpozembea huduma kwa wagonjwa”

Kiswaga ameyasema hayo Leo Septemba 11, 2024 wakati akipokea msaada wa vifaa tiba kutoka kwa Benki ya NMB, kwa ajili ya kusaidia huduma kwa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli iliyoko Mkoani Arusha.

“Nataka usafi uimarishwe na huduma bora ili hata wananchi wanaokuja kupima wakiona hivyo watamani kuumwa ili walale hapa hospitalini kutokana na hewa na mazingira mazuri pia masafi kuliko hata majumbani mwao” amesema Kiswaga.

Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, George Kasibante alishukuru NMB kwa msaada huo na kuahidi kuutunza ili ilete manufaa kwa wagonjwa na hospitali kwa ujumla.

Amesema kuwa msaada huo utaongeza wigo wa huduma kwa wagonjwa hasa wa kulazwa baada ya awali kufanikisha ukarabati na ujenzi wa majengo matano kupitia fedha za serikali walizoletewa zaidi ya Sh 500 milioni.

“Hivi karibuni serikali imetuletea zaidi ya Sh500 milioni ambayo imekarabati majengo yetu na kujenga mapya matano ya kufulia, upasuaji na mionzi lakini ofisi ya madaktari bingwa”

Amesema maboresho hayo yameenda sambamba na kuleta madaktari bingwa wa wanawake, macho na meno lakini pia imepunguza usumbufu wa rufaa kwa wagonjwa waliokuwa wanapelekwa Arusha Kutibiwa.

“Pia imeongeza wigo wa kuhudumia wagonjwa kutoka 80 hadi 100 lakini pia wakulazwa kutoka 80 hadi 120 kwenye vitanda 109 vilivyopo”

Awali akikabidhi misaada hiyo, Mkuu wa Idara ya Huduma za Kibenki kwa Serikali na Ofisi ya Makao Makuu ndogo ya NMB-Dodoma, Vicky Bishubo amesema, lengo la msaada huo ni kurahisisha utoaji huduma za afya kwa wananchi wanaofika kutibiwa katika hospitali hiyo ya Wilaya.

Amesema Vifaa hivyo ni mashuka 100, viti mwendo (2) chuma za kutundikia dripu (5) pamoja na Vitanda na magodoro (8) ikiwemo vitanda vitano vya  kulaza wagonjwa na vitatu vya kuwapumzisha kwa ajili ya vipimo vyote vikiwa na thamani ya Sh 6.5 milioni.

 “Ni desturi ya Benki yetu kujipambanua katika mambo ya kijamii, ndio maana tulivyopata barua ya maombi ya vifaa hivi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Monduli, tuliipa kipaumbele ya kuhakikisha tunafanikisha hitaji hili na leo tumekuja kukabidhi”

Amesema kuwa nia ya benki ya NMB ni kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwahudumia wananchi, ambapo mbali na gawio wanalotoa linaloelekezwa kwenye shughuli za maendeleo lakini pia wamekuwa wakitoa misaada mbali mbali.

“Kama Benki tuna vipaumbele katika misaada yetu hasa kwenye sekta muhimu za Afya, na Elimu lakini pia kutoa afueni kwa wanaokumbwa na majanga kama mafuriko, na moto lakini pia tuna kapeni ya utunzaji wa mazingira kupitia upandaji wa miti” amesema Bishubo.

Nae Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus amesema kuwa katika kuendelea kuwahudumia wananchi, Taasisi hiyo imeendelea kuwa wabunifu wa bidhaa zenye kutatua changamoto za kifedha kwa jamii ikiwemo mikopo ya riba nafuu.

Share To:

Post A Comment: