Katika kuendelea kuboresha maisha ya wananchi Vijijini, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetumia zaidi ya Shilingi Bilioni 100 kutekeleza miradi ya kupeleka umeme vijijini katika Mkoa wa Kigoma.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 18 Mkoani Kigoma wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu wakati wa ziara ya Bodi hiyo kukagua utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kupeleka umeme vijijini.

Wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti Kingu amewataka wakandarasi kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo kwa wakati uliopangwa, na kwamba hawatasita kuwachukulia hatua za kimkataba mkandarasi yoyote atakayeshindwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati kama ilivyopangwa.

“Tumeshatoa maelekezo. Hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa kwa mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi wake ndani ya muda uliopangwa, labda kwa sababu maalum.

Tumewaelekeza wakandarasi pia wahakikishe material yote yanayohitajika kama nguzo kabla ya msimu wa mvua kuanza ili miradi hiyo isichelewe kama ilivyo dhamira ya serikali umeme kuwafikia wananchi wote ndani ya muda,” amesisitiza Mwenyekiti Kingu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Radhia Msuya amesema kuwa ziara hiyo ni muendelezo wa ziara za Bodi hiyo kuhakikisha inatembelea miradi inayosimamiwa na REA kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kubadilisha hali za wananchi wa vijijini kama ilivyo adhma ya serikali.

Akizungumza awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa katika mkoa wa Kigoma, jumla ya Vijiji 279 kati ya Vijiji 306 katika Mkoa wa Kigoma tayari vimeunganishwa na nishati ya umeme na kusisitiza kuwa safari ya kupeleka umeme katika Vitongoji imeanza.

“Zaidi ya vitongoji 595 wakandarasi wanaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme. Katika vitongoji 1849 katika Mkoa wa Kigoma, vitongoji Zaidi ya 1370 tayari vimeshapata umeme. Tunaendelea kuhamasisha wananchi kuendelea kutumia miradi hii kutekeleza na kubuni shughuli za kiuchumi zitakazoweza kuboresha uchumi wao pamoja na kulinda miradi hii maana serikali imewekeza fedha nyingi sana,” amesema Mhandisi Saidy.









Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: