Na Asia Singano, WF-Morogoro

 
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, amewataka Watanzania kutumia Takwimu rasmi katika mipango na shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kupunguza athari zinazotokana na kufanya mipango ya maendeleo bila kuzingatia takwimu.

Dkt. Mussa aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Kikanda, Kanda ya Pwani, kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura No. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura No 103 na matumizi ya Takwimu rasmi zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu Kanda ya Pwani, uliyofanyika mkoani Morogoro.

Aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu ikiwemo vijana, wanawake, watu wenye ulemavu katika masuala ya Ununuzi wa Umma ili kuwainua na kuendelea kukuza uchumi.

"Ni vyema watu wa ununuzi waendelee kutoa fursa kwa makundi maalumu katika masuala ya ununuzi ikiwemo kuwaelimisha kuhusu fursa ziizopo katika ununuzi wa umma’’ Alisema Dkt. Mussa.

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel, alisema katika sheria ya ununuzi wa umma namba 10 ya mwaka 2023, Serikali imeweka fursa nyingi kwa ajili ya watu na kampuni za ndani ikiwemo kutenga zabuni takribani bilioni 50 ili kuongeza kipato kwa wananchi na kukuza uchumi wa nchi.

"Fursa hizo ni pamoja na kutenga zabuni za mpaka bilioni 50 kwa ajili ya Watanzania, kwa kazi za ujenzi, ununuzi wa bidhaa pamoja na huduma mbalimbali, kampuni zetu za ndani zimepewa fursa ya kuungana na kampuni za Nje au kuingia ushirika na kampuni za Nje ili kujenga uwezo wa kufanya kazi na zitakuwa kampuni kiongozi’’ Alisema Bi. Vicky.

Naye Afisa Ugavi Mkuu, kutoka Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Wizara ya Fedha, Bi. Fatuma Msantu, amewataka Wakuu wa Mipango pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Ununuzi kufuata sheria za ununuzi wa Umma na kutumia mfumo mpya wa Kielektroniki wa Manunuzi ya Umma (NeST).

"Na waachane na zile tabia za kutokutumia (NeST), ni muhimu, lazima waitumie ambapo pia itaweza kuwachukua hata wale wazalishaji wadogo ambao nao tunawahimiza waingie kwenye NeST ili waweze kuonekana wakati wazabuni wanapokwenda kwenye hizo zabuni zao’’ Alisema Bi.  Msantu.

Kabla ya Mikutano ya Kikanda inayoendelea kufanyika, ulianza mkutano kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta  Binafsi na Matumizi sahihi  ya Takwimu rasmi kwa Wakuu wa mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Mikoa, na Waganga Wakuu wa Wilaya Jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi  alikuwa Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck nchemba (Mb).
Share To:

Post A Comment: