Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kutenga fedha za mapato ya ndani zaidi ya Sh.Milioni 600 na kujenga Shule ya Msingi ya mchepuo wa Kingereza ya Chief Zulu.

Mhe. Rais ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na wazazi na wanafunzi baada ya kuzindua shule hiyo leo Septemba 24, 2024 Manispaa ya Songea.

“Nawapongeza sana Manispaa ya Songea kwa kutenga fedha zaidi ya shilingi milioni 600 kutoka kwenye mapato yenu ya ndani na kuamua kujenga shule hii muhimu kwa taaluma ya watoto wa Mkoa wa Ruvuma; Nimefarijika kuona mmejenga kuanzia madarasa ya awali ambayo yanawasaidia watoto kwenye malezi na makuzi bora kabla hawajaanza darasa la kwanza,”amesema.

Aidha amewataka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI kutafuta walimu wabobevu wa kufundisha Lugha ya Kingereza ili watoto hao waijue lugha hiyo kwa ufasaha.

“Shule kama hizi zinazofundisha Kingereza mnatakiwa kuweka walimu wanaoijua lugha hii vizuri ili kuwanoa watoto hawa kuwa mahiri kwenye lugha ya Kiingereza na sio kingereza cha kubabaisha,”amesema.

Aidha Mhe. Rais amesema kuwa serikali itaendelea kuboresha Sera ya Elimu ili kuendana na mabadiliko ya Dunia hivyo kwa sasa.

“Manavyoendelea kuongeza shule za michepuo ya Kingereza msisahau lugha yetu ya Kiswahili lakini pia mkaangalia lugha nyingine tunayoweza kuwafundisha watoto wetu ambayo ni fursa huko Duniani kama Kichina, Kifaransa nk…Katika hili mnaweza kugawa Mikoa kwa Kanda hivyo Mikoa kadhaa ikawa na shule za kufundisha Kingereza na lugha nyingine muhimu ya Kimataifa na shule za Mikoa mingine nazo zikafundisha Kiingereza na somo lingine ili tuweze kuwa na wataalam wengi wa lugha wanaoweza kupata soko kimataifa,”amesema.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hadi sasa nchini shule hizo za Mchepuo wa Kingereza ziko 68 ambazo zinafundisha lugha ya Kingereza.

Shule ya Chifu Zulu ina wanafunzi wa awali na Msingi 491 na wanafundishwa masomo yote kwa lugha ya kingereza isipokuwa kwa somo la Kiswahili.







Share To:

Post A Comment: