Jeshi la polisi nchini Tanzania limepiga marufuku maandamano
yaliyokuwa yamepangwa na chama cha upinzani Chadema kufanyika jijini Dar es
Salaam tarehe 23 Septemba 2024.
Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime ametoa onyo kwa
viongozi wa Chadema kuacha kuendelea kuwahamasisha wananchi kujihusisha kwa
kile alichokiita ni uhalifu
“Jeshi la polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa,
kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano
hayo asitubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika”
amesema Misime.
Siku ya Jumatano (11 Septemba 2024), Mwenyekiti wa Chadema
Freeman Mbowe alisema nia ya maandamano hayo ni kudai uhai wa wanachama na
viongozi mbalimbali wa chama hicho waliopotezwa.
Hata hivyo Misime ameonya kwamba waliopanga kuhudhuria
wasipoteze muda na gharama zao kwani yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa
vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania CCM
Dkt Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kinalaani utekaji na mauaji nchini
humo. Dkt Nchimbi amesema mauaji ya hivi karibuni ya kiongozi wa Chadema
Mohammed Kibao ni jambo la kusikitisha na linatia hofu kwa wananchi.
“Taifa linapita kwenye mtihani wa hofu miongoni mwa wananchi,
na hatuwezi kulipuuza hilo… Mtu yeyote anayehatarisha usalama wa raia, mtu
yeyote ama kikundi kinachotekeleza matendo ya utekaji hawawezi kuwa na nia
njema na CCM,” amesema Nchimbi.
Awali Mbowe alitoa siku kumi – hadi kufikia tarehe 21 Septemba
2024 – akitaka viongozi husika kuwajibika kwa tuhuma za watu kutekwa na kupotea
katika mazingira ya kutatanisha na kuonya hilo lisipofanyika wanachama na
viongozi wa Chadema wataandamana.
Hatahivyo, Nchimbi anasema msimamo wa Mbowe na Chadema ni
ushindi kwa genge la watekaji. “Tumemsikia Mbowe akitoa mud awa mwisho, yaani
tarehe 23 serikali isipotaja majina watachukua hatua. Kwa mtu kama Mbowe kama
kafikishwa hapo na genge la watekaji maana yake ni kuwa genge limefanikiwa.”
‘Genge la watekaji lina nia mbaya’
Nchimbi amedai kuwa matendo ya utekaji yanafanya na watu wenye
nia mbaya ya kufarakanisha taifa. “Jambo la utekaji na mauaji linatoa taswira
mbaya kwa CCM. Hivyo hatuwezi kuunga mkono.”
Nchimbi amasema tayari matendo hayo yanafanya raia wasiwe na
imani na polisi, na ameonya hilo likendelea litaathiri usalama na ustawi wa
nchi kwa ujumla. “Ni muhimu sisi pamoja na wapinzani kushirikiana ili tusiwape
genge la watekaji ushindi. Genge linataka kutufarakanisha.”
Kiongozi huyo amesema CCM inaunga mkono kauli ya rais Samia
Suluhu Hassan kutaka uchunguzi ufanyike. “Niseme kuwa CCM imekerwa kweli kweli
na jambo hili… Genge hili la watekaji linaweza kuwa popote, ndani ya CCM,
polisi au hata Chadema. Muhimu ni kuacha uchunguzi wa kina ufanyike, na majibu
yake yapatikane ili hatua zichukuliwe.”
Kuhusu hoja ya Chadema ya kutaka uchunguzi uongozwe na
makachero kutoka mashirika ya kijasusi ya kimataifa kama Scotland Yard ya
Uingereza, Dkt Nchimbi amesema CCM itaiunga mkono serikali kama itaona umuhimu
wa kushirikisha mashirika ya kimataifa.
Hata hivyo, Nchimbi amesema misimamo ya Chadema ya kutaka Rais
Samia ang’oke madarakani haiwezekani kwa kuwa yupo madarakani kikatiba na
ataondoka pale tu muda wake kikatiba utakapotamatika.
Post A Comment: