Waziri wa Madini Anthony Mavunde amepiga marufuku biashara ya madini kufanyika majumbani kwa watu na kusisitiza kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili kudhibiti utoroshaji madini na upotevu wa mapato ya Serikali.

Amesema hayo leo Septemba 17, 2024 Wilayani Tunduru, Ruvuma akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo kukagua miradi na maendeleo ya shughuli za madini ambapo ametembelea na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Soko la Madini Wilaya ya Tunduru na kuipongeza Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kushirikiana na wafanyabiashara kufanikisha ujenzi wa soko hilo kubwa lenye kukidhi mahitaji.

Mhe. Mavunde ametoa maelekezo ya kuhakikisha biashara yeyote ya madini kufanyika katika eneo moja na rasmi (One Stop Centre) na kwamba Soko hilo lina mifumo bora na miundombinu yanayotakiwa kwa mujibu wa Sheria ili kudhibiti na kuziba mianya ya udanganyifu na utoroshaji wa madini kwa manufaa ya taifa na wananchi wake.

“Nitoe maelekezo hapa, ni marufuku biashara yeyote ya madini kufanyika nje ya Soko la Madini, Serikali imeweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara ya madini kwa uwazi ili kudhibiti mapato ya Serikali, kukuza sekta, na kuongeza mchango wa Sekta katika Pato la Taifa” amesema Mavunde. 

“Tutaleta kikosi kazi (task force) hapa na kufanya operesheni maalum ya kudhibiti na kuwabaini watu wote wanaofanya biashara za kununua madini majumbani ili wakafanye  shughuli zao kwenye Soko rasmi la madini, na tutachukua hatua kali za kisheria kwa wote watakaokaidi agizo hili" ameongeza Mhe. Mavunde. 

Amesema kuwa, kwa mfanyabiashara yeyote atayekamatwa akifanya biashara ya madini majumbani atafutiwa leseni yake, madini hayo yatataifishwa na hataruhusiwa tena kufanya shughuli za madini popote nchini Tanzania.

Aidha, Waziri Mavunde amesema kuwa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha watu wote waliopo kwenye mnyororo mzima wa shughuli za madini wananufaika na rasilimali hiyo kwa kutenda haki wakiwemo Wachimbaji Wadogo na hatimaye kuongeza mchango wao katika maendeleo ya sekta, mapato yao na ya Serikali pamoja na uchumi kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amepiga marufuku Wafanyabiashara raia wa kigeni kwenda kununua madini machimboni badala yake wafanye shughuli za biashara zao kwenye masoko rasmi na si vinginevyo kwa kuwa ni kinyume na Sheria ya Madini Sura ya 123.

Awali, akiwasilisha taarifa ya Ujenzi wa Soko hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Bw. Chiza Malando amesema Ujenzi wa Soko hilo utagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 2.1 hadi kukamilika kwake, wafanyabiashara wakichangia shilingi bilioni 1.085 huku Halmashauri ikitoa eneo na ramani yenye thamani ya shilingi bilioni 1.065 kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha amesema kuwa Ujenzi wa Soko hilo la pamoja utasaidia kuongeza uwazi katika biashara ya madini pamoja kuongeza ufanisi katika suala la ulinzi na usalama ili kudhibiti utoroshaji madini hatimaye kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali. 

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini Mhe. Hassan Zidadu Kungu na Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Mhe. Daimu Mpakate wameishukuru Serikali kwa usimamizi mzuri Sekta ya Madini na kwamba lengo ni kuona rasilimali ya madini inaleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Share To:

Post A Comment: