Mkurugenzi wa Jiji la Tanga, Mhandisi Juma Hamsini, leo Jumatatu, Septemba 23, 2024, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya sekta ya elimu sekondari, kuangalia hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi, na kuondoa changamoto zinazochelewesha ukamilishaji wa miradi hiyo.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Hamsini alianza kwa kutembelea ujenzi wa mabweni mawili katika shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga, Tanga Technical Secondary School, ambayo yapo kwenye hatua za umaliziaji, yanayojengwa kwa fedha za Mradi wa Programu ya Kutekeleza Elimu kwa Matokeo (EP4R) kwa gharama ya shilingi milioni 260, na uwezo wa kulala jumla ya wanafunzi 160.
Akiwa shuleni hapo, Mhandisi Hamsini alisisitiza kukamilika kwa kazi ndani ya muda na wanafunzi kuhamia kwenye mabweni hayo kama ilivyopangwa, na amepongeza hatua za umaliziaji zilivyofikia.
Mhandisi Hamsini pia ametembelea shule za Sekondari za Msambweni, Galanos na MACECHU, ambapo katika shule zote hizo, ameweza kukagua miradi ya ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, Bweni na nyumba za watumishi, ambavyo vinajengwa kwa fedha za Serikali Kuu na mapato ya ndani, na kutoa maelekezo kwa Mhandisi na Mchumi wa Jiji kuhakikisha wanapeleka nguvu ya kukamilisha miradi hiyo ili iweze kutoa huduma kwa jamii.
Ziara hii ya kutembelea miradi ya sekta ya elimu ni ya pili kwa Mkurugenzi Hamsini, tangu ahamie Jiji la Tanga, ambapo ziara yake ya kwanza alianzia kwenye sekta ya afya, aliyoifanya kwa siku mbili, kuanzia Septemba 17, 2024, na alitembelea na kukagua miradi 11.
Post A Comment: