Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kusaini Mkataba wa Ujenzi wa Daraja katika eneo la Jangwani jijini Dar es salaam ambapo mkataba unatarajiwa kuwa umesainiwa mwezi Septemba, 2024.

Bashungwa ameeleza hayo leo Septemba 02, 2024 jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga aliyehoji Lini Serikali itaanza rasmi ujenzi wa Daraja la Jangwani kuanzia Magomeni-Jangwani-Fire ili kuondoa adha wanayopata wananchi wakati wa mvua?

“Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imepanga kujenga Daraja katika eneo la Jangwani lenye urefu wa mita 390 na kimo cha mita 15 ambapo hivi sasa taratibu za manunuzi zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wake”, ameeleza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa Daraja la Jangwani utatumia fedha za mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa ujenzi wa Daraja la Jangwani utaenda sambamba na zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais - TAMISEMI kupitia mradi wa Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi (DMDP II).

Katika hatua nyingine, Bashungwa ameeleza kuwa tayari Wizara ya Ujenzi imeanza kupokea fedha kutoka Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ya awali kwa Wakandarasi ambao walikuwa wakisubiria fedha hizo ili waweze kuendelea na utekelezaji wa miradi ya ujenzi ya barabara na madaraja inayoendelea na kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge fedha hizo zitaanza kutolewa mara moja ili kazi ziendelee.

Share To:

Post A Comment: