Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango amefungua mkutano wa 35 wa kamati ya kudumu ya fedha ya mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, akisema uamuzi wa kuchagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaenda sambamba na dhamira ya Tanzania katika ufadhili wa kijinsia kwaajili ya mabadiliko ya hali ya hewa nchini.


Mhe. Mpango katika mkutano huo unaofanyika Jijini Arusha kwenye kituo cha mikutano cha AICC na kushirikisha wajumbe zaidi ya 200 kutoka nchi 80, ameipongeza pia kamati hiyo ya fedha kwa kusaidia uwiano na uratibu wa jitihada mbalimbali za udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi katika kutekeleza makubaliano ya mkataba wa kimazingira wa Paris.


Akizungumzia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa Tanzania, Dkt. Mpango ameyataja mafuriko yaliyotokea Hanang Mkoani Manyara Disemba 2023 na kuua takribani watu 89, majeruhi na makazi kuharibika pamoja na uharibifu wa mitandao ya barabara za kitaifa kwa takribani Km. 520 uliojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini.


Amekumbusha umuhimu wa usawa katika kukabiliana na masuala ya mabadiliko ya tabianchi, akisema Tanzania imeendelea kuhimiza ujumuishaji wa masuala ya jinsia na mabadiliko ya tabianchi kwenye sera, programu na mikakati yake katika ngazi mbalimbali za kiuongozi.


Kaulimbiu ya mkutano huo inasema "Kuongeza kasi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia ufadhili unaozingatia Jinsia"

Share To:

Post A Comment: