Katika hali inayoleta maswali na sintofahamu wanachama na wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) unaweza kusema wamemsusia Mwenyekiti wa chama hicho Taifa Freeman Mbowe katika kushiriki maandamano yaliyopangwa kufanyika leo, Jumatatu Septemba 23.2024 jijini Dar es Salaam


Licha ya ukweli kwamba kabla ya leo, kumeshuhudiwa mivutano baina ya CHADEMA, Jeshi la Polisi na serikali kwa ujumla ambapo mivutano hiyo imetokana na Jeshi la Polisi kuweka ngumu maandamano hayo jambo ambalo lilipingwa vikali na CHADEMA ambapo kupitia Mbowe waliahidi lazima waingie barabarani kuandamana.

Polisi walitanda maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam na miji mikuu wakionyesha uimara wa kulinda amani, huku ikionesha wazi kutokua na muitikio kutoka kwa wananchi na hata wafuasi wa Chadema kama ilivyotarajiwa. Baadhi ya wananchi wamesema wafusi wengi wameandamana kwenye mitandao.

Wadau mbalimbali hapa nchini na pengine hata nje ya mipaka ya Tanzania waliokuwa wanaofuatilia sakata hilo walitarajia pengine kuona idadi kubwa ya wafuasi wa chama hicho wakijitokeza barabarani kama sehemu ya hatua ya kuunga mkono viongozi wa kitaifa wa chama chao waliokuwa wamesita kujitokeza kushiriki maandaman .

Katika kile ambacho unaweza kutafsiri kama usaliti kwa Mwenyekiti wao wa Taifa, viongozi wengi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA hawajajitokeza barabarani tofauti na ilivyotarajiwa hapo awali, au kama ilivyoshuhudiwa hamasa iliyojitokeza kwenye mitandao ya kijamii kabla ya leo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya nje John Mrema iliyoeleza kulaani kushikiliwa kwa baadhi ya viongozi na wanachama wao leo, Jumatatu Septemba 23.2024 imeonesha kuwa wanachama wasiozidi 50 wanashikiliwa na Polisi, ambapo kati ya hao wapo baadhi ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho, lakini polisi ilitoa orodha ya watu 14 iliyowakamata.

Hadi sasa viongozi waliothibitika kukamatwa ni pamoja na Freeman Mbowe mwenyewe, Makamu Mwenyekiti CHADEMA Tanzania Bara Tundu Lissu, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Tanzania Bara Benson Kigaila, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini Godbles Lema na wengineo
Share To:

Post A Comment: