Na Asia Singano, WF- Kilimanjaro


Maafisa Ununuzi wa Umma nchini wametakiwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Ununuzi wa Umma ili kufikia malengo ya mabadiliko ya Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma ikiwa ni pamoja na kuwanufaisha wazawa.

Rai hiyo ilitolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Kiseo Yusuf Nzowa, wakati akifungua mkutano wa Kikanda, Kanda ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura No. 410, Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, Sura No 103 na matumizi ya Takwimu rasmi zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Kanda ya Kaskazini, uliyofanyika mkoani Kilimanjaro.

Aliongeza kuwa kutokana na fursa zilizopo katika Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sheria hiyo italeta tija endapo watu wanaohusika na masuala ya ununuzi wa Umma wataifuata sheria hiyo na taratibu zote za ununuzi wa Umma.

‘’Tumeona mabadiliko mazuri yaliyopo kwenye Sheria Mpya ya Ununuzi wa Umma, ambayo kwa kiasi kikubwa yananufaisha wazawa, wito wangu kwa wanaohusika na manunuzi waifuate Sheria hii’’ alisema Bw. Nzowa.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kaskazini, Bw. Magai Maregesi, amewashauri Watanzania kujisajili kwenye mfumo mpya wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST), ili kunufaika na Sheria hiyo inayotoa fursa za kiuchumi kwa wananchi wote wakiwamo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

‘’ Nawasihi Watanzania kuacha kukwepa Mfumo wa NeST kwa kuwa kuna fursa nyingi kwenye Sheria ya Ununuzi ikiwemo fursa za biashara na uwekezaji, bila kujisajili wazabuni hawatatambua uwepo wao kwa wepesi’’ Alisema Bw. Maregesi.

Kabla ya Mikutano ya Kikanda inayoendelea kufanyika, ulianza mkutano kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na Matumizi sahihi ya Takwimu rasmi kwa Wakuu wa mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Mikoa, na Waganga Wakuu wa Wilaya Jijini Dodoma hivi karibuni ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck nchemba (Mb).
Share To:

Post A Comment: