Msimamizi wa uchaguzi katika halmashauri ya Longido  iliyoko wilayani Longido Mkoa wa Arusha Nassor Shemzigwa ametoa mwongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024 unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu. 

Akizungumza na waandishi wa habari ameeleza hatua zitakazoongoza mchakato wa uchaguzi kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, uchukuaji na urejeshaji wa fomu za wagombea, uteuzi wawagombea na tarehe ya siku ya uchaguzi una lengo la kutoa mwongozo mzuri utakaohakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na usawa kwa kuzingatia Sheria na taratibu zilizowekwa.

Hata hivyo amesema lengo ni kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa lakini pia wagombea na wapiga kura wanapata taarifa zote zinazohitajika kwa wakati.


Sambamba na hilo ameongezea kuwa wanaoruhusiwa kugombea nafasi za wenyeviti na wajumbe Shemzigwa amesema ni Watanzania wenye akili timamu waliofikisha umri kuanzia miaka 21 na kuendelea huku wanaoruhusiwa kupiga kura ni wananchi wenye umri wa miaka 18 na kuendelea na ambao wameshiriki na watakaoshiriki zoezi la uandikishaji wa wapiga kura.

"Fomu za kugombea zitatolewa na kutakiwa kurudishwa kuanzia Novemba Mosi hadi saba mwaka huu kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambapo uteuzi utafanyika Novemba nane na siku hiyo tutaanza kupokea mapingamizi kuhusu uteuzi kwa siku mbili hadi Novemba 10" amesema Shemzigwa.


Amesema kuwa baada ya hapo wataanza kupokea rufaa na kutolewa maamuzi yake kuanzia Novemba 10 hadi 13.

"Baada ya mchakato huo wa uteuzi, kampeni rasmi za uchaguzi zitaanza Novemba 20 hadi 26 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12"

Amewataka wananchi wote wenye sifa kuhakikisha wanashiriki kwenye mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia hatua za uandikishaji kwenye orodha ya wapiga kura hadi upigaji wa kura.

"Nafasi zinazogombewa ni Mwenyeviti wa Vijiji, wajumbe watano ambao kati yao wajumbe wawili ni wanawake hivyo watu wote washiriki ili kukuza demokrasia na kuhakikisha upatikanaji wa viongozi bora kwa maendeleo ya Taifa" amesema Shemzigwa.
Share To:

Post A Comment: