Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo Husna Sekiboko ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hssan kwa uamuzi wake wa kujenga ofisi na maabara za Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Zanzibar jambo litakalosaidia upimaji wa sampuli mbalimbali pamoja na kusaidia watafiti kuitumia maabara hiyo.

SEKIBOKO ameyasema hayo baada ya ziara ya kamati ya kudumu ya bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo kutembelea ofisi na maabara za TAEC eneo la Dunga Zuze Zanzibar ambapo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100 kwa sasa usimikaji wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa vya maabara unaendelea.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mh. Omary Kipanga amesema katika mchakato wa uzalishaji bidhaa pamoja na chakula suala la mionzi haliwezi kuepukika kwa kuwa vyakula vinavyoingizwa ndani ya nchi na vinavyotoka nje ya nchi ni lazima viratibiwe vizuri ili visiwe na athari za mionzi hivyo uwepo wa maabara ya upimaji wa mionzi Zanzibar kunaimarisha usalama wa wananchi pamoja na mazingira .

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Prof. Najat Kassim Mohammed amesema ofisi na maabara za TAEC Zanzibar zimejengwa eneo maalum la kimkakati la viwanda hivyo bidhaa zinazohitaji kupimwa mionzi zitapimwa katika maabara hiyo jambo litakalorahisisha utendaji.

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo inetembelea miradi mbalimbali ya kimkakati nchini kwa lengo la kuona namna fedha zinazotolewa na serikali baada ya kupitishwa na bunge zinavyotumika kwa maslahi ya taifa.








Share To:

Post A Comment: