Jamii ya Wahadzabe na Wagatoga ni moja kati ya makabila machache yaliyobaki kote duniani yanayoendeleza utamaduni wa kale, ikiwa ni pamoja na shughuli za uwindaji na maisha ya kula matunda, mizizi na aina mbalimbali za wanyama wa porini kwa miaka zaidi ya elfu 40 hivi sasa wakiishi na wanyama tofauti kabisa na unavyoweza kudhani.
Licha ya kuishi Pembezoni kabisa mwa Mkoa wa Arusha na wilaya ya Karatu, Serikali ya Halmashauri ya Wilaya haijawaacha nyuma katika kuwashirikisha programu na mipango mbalimbali ya kijamii, kidemokrasia pamoja na ushiriki wao kwenye kuamua mambo yao, kuchagua na kuchaguliwa kwenye nafasi mbalimbali za Kiuongozi.
Kilomita zaidi ya 35 kutoka Karatu Mjini, Vilima, vichaka na mabonde, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Ndugu Juma Hokororo, amefika mpaka Kijijini Mang'ola kukutana na Jamii hizi na dhamira kubwa ni kutoa elimu kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na kuhamasisha Jamii hizo kuweza kushiriki kwenye mchakato huo muhimu kidemokrasia na kichocheo kikubwa cha maendeleo yao binafsi.
"Nimekuja kuwaambia na kuwahamisha kushiriki kwenye kugombea nafasi mbalimbali za Uongozi. Tungefurahi kuwaona watu wa Jamii hii ya Kihadzabe kwenye nafasi mbalimbali za Uongozi. Twendeni tuhamasishane kugombea na tukachague viongozi wanaotufaa kwa maendeleo ya Mang'ola." Amesema Ndugu Hokororo.
Post A Comment: