Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.
Doto M. Biteko, Septemba 19, 2024 anatarajia kuwa mgeni rasmi katika hafla ya
uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme
katika Mto Malagarasi wa megawati 49.5, njia
ya kusafirisha umeme ya msongo wa
Kilovoti 132 kutoka Igamba hadi Kidahwe
yenye urefu wa Kilomita 54 na Kituo cha kupoza na kusambaza umeme msongo wa
kilovoti 400/220/132/33 cha Kidahwe mkoani Kigoma.
Katika utekelezaji wa mradi wa Malagarasi,
utagharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 144.14 (sawa na shilingi za
Tanzania bilioni 388) ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itagharamia kiasi cha dola za Marekani milioni 4.14 na benki ya Maendeleo ya
Afrika-AfDB inagharamia kiasi cha dola za
Marekani milioni140 kama mkopo wenye masharti nafuu.
Mradi utahusisha sehemu kuu tatu ambapo sehemu ya
kwanza itahusisha Ujenzi wa Bwawa
la kuzalisha umeme ikiwemo tuta (Dam),
njia za kupitisha maji (Waterways),
jumba la mitambo ya kufua umeme (Powerhouse)
lenye uwezo wa kuzalisha Megawati 49.5 pamoja na kituo cha kupokea umeme na kuuongezea
nguvu wa msongo wa kilovoti 132 (Switchyard);
Sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa njia ya
kusafirisha umeme wa Msongo wa kilovoti 132 (Transmission Line) yenye urefu wa km 54 ambayo itaunganisha Kituo
cha kuzalisha umeme na Gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupoza umeme cha
Kidahwe;
Na sehemu ya tatu inahusisha ujenzi wa mtandao wa
usambazaji umeme katika vijiji saba (7) vinavyopitiwa na mradi ambavyo ni
Mazungwe, Kidahwe, Mwamila, Kalenge, Kazuramimba, Mlela na Igamba.
Mradi wa Malagarasi
unatarajiwa kuzalisha umeme wa wastani wa Gigawati hour 181 kwa mwaka. Umeme
huu utasaidia mahitaji ya ndani ya mkoa wa Kigoma, mikoa ya jirani pamoja na
kuwezesha biashara ya umeme kikanda (Southern and Eastern Africa Power Pools),
pamoja na kuboresha huduma za kijamii ikiwemo
Elimu, Afya, maji pamoja na biashara za viwanda.
Imetolewa na;
Neema Chalila Mbuja,
Kaimu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.
WIZARA YA NISHATI
Post A Comment: