Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Arusha DC, iliyoko Wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Selemani Msumi ametangaza mapema watu watakaoruhusiwa kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa kwa mwaka 2024.
Amesema kuwa wenye sifa ya kugombea na nafasi za serikali za mitaa, lazima awe Raia wa Tanzania na mkazi wa eneo husika analogombea tena awe na umri kuanzia miaka 21 na kuendelea.
Sifa zingine, Msumi amesema Mgombea lazima awe na akili na timamu na awe alimepewa dhamana au mwanachama wa Chama wa siasa na zaidi awe na shughuli za kujipatia kipato lakini pia aweze kuandika na kusoma lugha ya Kiswahili au Kingereza.
Msumi ambae pia ni Mkurugenzi wa halmashauri wa Arusha Meru, ameyasema hayo wakati akitoa maelekezo ya uchaguzi wa serikali za mitaa Leo Septemba 26,2024 ikiwa ni siku 62 kabla ya siku ya uchaguzi huo Novemba 27 mwaka huu.
Mbali na hilo amesema wapiga kura watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale Watanzania waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura na wakazi wa eneo husika lakini waliofikia umri wa miaka 18 na kuendelea na zaidi wawe na akili timamu.
"Fomu za kugombea zitatolewa na kutakiwa kurudishwa kuanzia Novemba Mosi hadi saba mwaka huu kwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi ambapo uteuzi utafanyika Novemba nane na siku hiyo tutaanza kupokea mapingamizi kuhusu uteuzi kwa siku mbili hadi Novemba 10" amesema Msumi.
Amesema kuwa baada ya hapo wataanza kupokea rufaa na kutolewa maamuzi yake kuanzia Novemba 10 hadi 13.
"Baada ya mchakato huo wa uteuzi, kampeni rasmi za uchaguzi zitaanza Novemba 20 hadi 26 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 hivyo niwaombe wananchi wenye sifa hizo hapo juu wahakikishe wanashiriki mchakato mzima hadi kupatikana viongozi wenye sifa" amesema Msumi.
Amesema nafasi zinazogombewa ni Mwenyeviti wa Mtaa, na vitongoji, wajumbe watano ambao kati yao wajumbe wawili ni wanawake hivyo kuwataka watu wote washiriki Ili kukuza demokrasia na kuhakikisha upatikanaji wa viongozi Bora kwa maendeleo ya Taifa" amesema Msumi.
Post A Comment: