Na. James K. Mwanamyoto, OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameitaka Wakala wa Mabasi yaendayo kwa Haraka (DART) kuhakikisha wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanapata kadi janja kwa urahisi na kuanza kuzitumia kwa ajili ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi.

Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam, wakati akizindua matumizi ya mageti janja na kadi janja kwa ajili ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi katika jiji hilo ambalo lina uhitaji mkubwa wa usafiri wa mabasi yaendayo kwa haraka.

Waziri Mchengerwa amesema kuwa, mara baada ya uzinduzi alioufanya hategemei kusikia kituo chochote cha mwendokasi jijini Dar es Salaam kinaendelea kutumia tiketi za makaratasi badala ya kutumia kadi janja ambazo zitawaondolea hadha ya foleni wananchi wanaotumia usafiri wa mwendokasi.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema matumizi wa kadi janja yataongeza usafi wa mazingira katika jiji la Dar es Salaam na kuongeza kuwa Ofisi ya Rais - TAMISEMI yenye dhamana ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya DART imejipanga kuhakikisha wananchi wananufaika na matumizi ya kadi janja. 

“Nailekeza DART kuhakikisha kadi janja zinapatikana kwa urahisi jijini Dar es Salaam na kusiwepo na changamoto ya wananchi kuzipata kadi janja kwa ajili ya usafiri wa mabasi ya mwendokasi,” Mhe. Mchengerwa alisisitiza.

Sanjari na hilo, Mhe. Mchengerwa ameitaka DART kumaliza changamoto zinazowakwamisha wakazi wa jiji la Dar es Salaam kushindwa kutumia vizuri usafiri wa mwendokasi, ikizingatiwa kuwa tayari ameshazindua kadi janja ambazo zitawarahisishia wananchi kutumia usafiri huo wa mwendokasi kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Share To:

Post A Comment: