Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dkt. Naomi Katunzi akiongea wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wajumbe wa Baraza hilo lililomaliza muda wake Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam  Septemba 25, 2024. Kushoto ni aliyekuwa Makamu wake, Prof. Sotco Komba.

Aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) lililomaliza muda wake, Bibi Theresia Mbando akitoa nasaha kwa viongozi na watumishi wa TEWW wakati wa hafla fupi ya kuwaaga iliyofanyika  Septemba 25, 2024, Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Michael Ng’umbi akiwakaribisha wajumbe wa Baraza la Usimamizi la Taasisi hiyo lililomaliza muda wake kwenye hafla fupi ya kuwaaga  Septemba 25, 2024, Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima lililomaliza muda wake wakiwa kwenye hafla fupi ya kuwaaga  Septemba 25, 2024, Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Sehemu ya wajumbe wa Menejimenti ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima wakiwa kwenye hafla fupi ya kuwaaga wajumbe wa Baraza la Usimamizi la Taasisi hiyo lililomaza muda wake Septemba 25, 2024, Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dkt. Naomi Katunzi (katikati) na aliyekuwa Makamu wake, Prof. Sotco Komba (kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu wa Baraza hilo, ambaye pia ni Mkuu wa TEWW, Prof. Michael Ng’umbi Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam  Septemba 25, 2024.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi la Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dkt. Naomi Katunzi (katikati) na Makamu wake, Prof. Sotco Komba (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza hilo, muda mfupi kabla ya hafla ya kuliaga Baraza hilo lililomaliza muda wake. Wa pili kulia ni Mkuu wa TEWW, Prof. Michael Ng'umbi, ambaye alikuwa Katibu wa Baraza hilo. Hafla hiyo imefanyika  Septemba 25, 2024, Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam


Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW)  Septemba 25, 2024 limetoa pongezi kwa uongozi wa taasisi hiyo kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria, miongozo na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kuwaaga wajumbe wa Baraza hilo lililomaliza muda wake, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Sotco Komba amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu ya uhai wa Baraza, TEWW imetekeleza majukumu yake ipasavyo, na wakati wote uongozi ulihakikisha unawasilisha masuala yote yaliyohitaji kupatiwa ufumbuzi na Baraza.

“Menejimenti imekuwa ikitekeleza majukumu yake kulingana na sheria, miongozo na taratibu...wamekuwa wakileta jambo lolote lile lililohitaji majadiliano zaidi kwenye Baraza na sisi tulikuwa tunalichakata na kutolea maamuzi...hivyo nitoe pongezi kwa kazi nzuri mliyokuwa mkiifanya,” amesema Prof. Komba.

Aidha, Prof. Komba ametoa wito kwa TEWW kuendelea kubaki kwenye ubora katika taaluma na kutenga fedha kwa ajili ya tafiti ili kuleta ushindani na taasisi nyingine zinazotoa wahitimu wenye sifa sawa za kitaaluma na kulinufaisha taifa.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dkt. Naomi Katunzi ameitaka TEWW kuongeza idadi ya kozi inazozitoa, kuwa na kozi za muda mfupi, kufanya tafiti na kutoa huduma ya ushauri elekezi ili kuongeza mapato ya taasisi.

“Jitahidini sana ku-diversify kozi zenu ili muwe na mapato makubwa...tafiti na ushauri elekezi ni vyanzo vikubwa vya mapato...angalieni sana eneo la short course,” amesema.

Sambamba na hilo, Dkt. Katunzi aliwaombea viongozi na watumishi wa TEWW baraka za Mwenyezi Mungu za upendo, furaha na amani; na kuwaasa kupendana, kutobaguana, kufanyakazi pamoja kirafiki na kuwa karibu na wizara mama ili wafanikiwe.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: