MENEJA wa Wakala wa Vipimo (WMA) Phanuel Matiko, akizungumza na waandishi wa habari katika banda la WMA kwenye maonesho ya wakulima kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
MENEJA wa Wakala wa Vipimo (WMA) Phanuel Matiko amesema ili wakulima kuepuka kipimo cha lumbesa wanatakiwa kuacha tabia ya kuuzia mazao yao Shambani.
Matiko ameyasema hayo leo Agosti 7,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wakulima kitaifa yanayofanyika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Amesema kuwa ili wakulima kuepuka kipimo cha lumbesa wanapaswa kuacha tabia ya uuzaji wa mazao yao ya kilimo shambani.
"Wito wangu niwaombe wakulima kuacha tabia ya kuuza mazao yao shambani ili kuepuka lumbesa bali watumie mizani kwa kuuza mazao yao kwa kilo.
"Wakulima hawapaswi kuuza mazao yao kwa kutumia debe au kisado au vitu vingine vinavyofanana na hicho bali watumie mizani ili kuepuka lumbesa kwenye uuzaji wa mazao yao,"amesema.
Amesema pia wao ni wadau wakubwa kutokana na jukumu lao la kupima usahihi wa mizani, mita za maji, umeme pamoja na pampu za mafuta.
"Moja ya majukumu yetu ni kupima usahihi wa mizani ili kile ambacho mtu atanunua kiwe kweli kinalingana na fedha yake lakini pia hivi sasa tunapima mita za umeme na maji.
"Tunakagua alichokitumia na kulipa kama ni sawa. Pia kwenye ukaguzi wa Pampu za mafuta tunakagua kiasi cha mafuta hivyo hata mkulima akipeleka trekta kujaza mafuta basi asiibiwe iwe kwenye ujazo sahihi,"amesema.
Hata hivyo amewahamasisha wakulima pamoja na wananchi kutembelea banda la WMA ili kupatiwa elimu mbalimbali inayohusu majukumu yao katika Wakala huo.
Post A Comment: