Eleuteri Mangi, Dar es Salaam


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amemwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kumchukulia hatua kali za kinidhamu Afisa Ardhi Mwandamizi Gaudence Mtalo kwa kusababisha mkanganyiko kwa kukosa uadilifu katika kutekeleza majukumu yake.

Waziri Ndejembi ametoa maelekezo hayo Agosti 15, 2024 jijini Dar es salaam wakati wa kikao chake na watumishi wa Ardhi Mkoa wa Dar es salaam na Pwani baada ya kusikiliza pande mbili zinazodai kumiliki kiwanja kilichopo Tegeta Wilaya ya Kinondoni, Dar es salaam ambacho mtumishi huyo anahusika katika mkanganyiko huo.

“Hatuwezi kuvumilia tabia za namna hii, ninyi ndiyo mnatuletea matatizo ya kuichafua Wizara, huu mkanganyiko umesababishwa na Afisa asiye mwadilifu na ndiyo wanatusababishia migogoro mingi, Afisa asiyefuata taratibu sisi hatuwezi kumvumilia” 

“Naelekeza ukaripoti ofisi za TAKUKURU ili uelezee umefikiaje maamuzi haya ya kutofuata taratibu lakini pia Katibu Mkuu akuchukulie hatua za kinidhamu” amesema Mhe. Ndejembi.

Waziri Ndejembi amezitaka pande mbili ambazo zinadai kila mmoja kuwa ni mmiliki wa kiwanja hicho ndugu John Nyoni na Ramadhani Salum Mwikalo kutoendelea na kazi ya kuendeleza eneo hilo hadi taratibu za kisheria zitakapokamilika na maamuzi yatatolewa na hatua zitazochukuliwa ili kumilikisha kiwanja hicho.

Aidha, Waziri Ndejembi amewataka maafisa ardhi kuwahudumia watanzania wanaofika kwenye ofisi hizo kwa weledi malalamiko ambayo yamekua yakitolewa na wananchi kwa idara za ardhi nchini.

Mhe Ndejembi pia amemtaka Msajili wa Hati kuongeza kasi ya kuwasikiliza watu hatua itakayosaidia kupata Hati Miliki Ardhi kwa wakati.   

Huo ni mwendelezo wa ziara za Waziri Ndejembi kuijua Wizara hiyo inavyofanyakazi katika sekta ya Ardhi ambayo ndiyo rasilimali inatumika na watu wote mijini na vijijini.

Share To:

Post A Comment: