Watumishi watatu wa halmashauri ya Wilaya ya Longido Mkoani Arusha wamekumbana na adhabu kali kutoka baraza la Madiwani ya kufukuzwa kazi, kushushwa cheo kwa kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya milioni 300.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi Halmashauri ya Longido ametiwa hatiani na Baraza la Madiwani kwa Uzembe kazini baada ya Kuisababishia Hasara ya milioni 335 kwa kushindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Longido.
UTATA MABILIONI UJENZI HOSPITAL LONGIDO
Kimoso ambaye kitaaluma ni Fundi ujenzi anadaiwa kushindwa kufanya makadirio sahihi ya vifaa vya ujenzi wa hospitali hiyo na kusabisha utofauti wa asilimia 15 ikiwa ni kinyume na sheria.
Baraza hilo limeazimia adhabu kwa mtumishi huyo ni kushushwa cheo, maamuzi hayo ni kulingana na Kanuni ya 42 (1) ikisomwa pamoja na kifungu cha 48 (3) cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022.
Lomnyaki Mollel, Tabibu Mkuu Daraja la Pili, yeye amekutwa na hatia ya upotevu wa dawa za Trakoma kopo 130, zenye thamani ya milioni nane, zilizokuwa zimehifadhiwa katika duka la Hospitali ya Wilaya ya Longido.
Adhabu yake ni Kupunguziwa msharahara kwa asilimia 15 kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Mtumishi mwingine Thomasi Mitiaki, aliyekuwa mtendaji Kata ya Olmologi amefukuzwa kazi kwa kukutwa na hatia ya ubadhirifu wa Mahindi ya Bei nafuu ya shilingi milioni 16 yaliyotolewa na Serikali, ambapo mtuhumiwa anadaiwa aligushi majina ya wanufaika.
Hata hivyo baraza hilo kupitia kwa Mwenyekiti wake Simon Laizer Katika kikao walichoketi Agosti 17, 2024, limetoa onyo kwa watumishi wengine watakaosubutu kuihujumu serikali kwani watakutana na mkono wa sheria.
Credit : Wasafifm
Post A Comment: