Na Ramadhani Kissimba

 
Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro, Bi. Ruth John amewaomba watalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na sekta ya fedha nchini kutatua changamoto zinazowakabili wananchi hasa watumishi wa umma zinazotokana na upatikanaji wa huduma za fedha zisizo rasmi.
 
Bi. Ruth aliyasema hayo wakati Timu ya program maalum ya elimu ya fedha kwa umma kutoka Wizara ya Fedha na washirika kutoka sekta ya fedha nchini walipofika ofisini kwake kabla ya elimu hiyo kutolewa kwa wakazi wa Morogoro mjini.
 
Bi. Ruth alisema kuwa suala la mikopo isiyofuata taratibu limekuwa na changamoto nyingi sana sio kwa wajasiriamali pekee bali hata kwa Watumishi wa Umma hii inatokana na uhitaji wa fedha maana kila mtu ana uhitaji wake.
 
‘’Changamoto tunazipata sana hadi kwa watumishi wa umma hususan walimu ambao wanaingia kwenye changamoto hiyo kwa sababu kila mtu ana uhitaji wake, na anapopata shida haaangalii kitu gani kipo mbele yake ambacho kitamletea madhara’’ Alisema Bi. Ruth
 
Bi. Ruth aliongeza kuwa kumekuwa na watoa huduma wengi wanaotoza riba kubwa ambayo wakati mwingine inazidi kiasi cha mkopo na Taasisi nyingi kati ya hizo hazijasajiliwa na wakopeshaji wengine wanawakopesha wananchi majumbani ambapo ni kinyume na utaratibu.
 
Kwa upande mwingine akizungumza katika program hiyo iliyotelewa kwenye ukumbi wa Mbaraka Mwinshee Mjini Morogoro, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa elimu ya fedha kwa umma ni matakwa ya Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha ambao unalenga kumlinda mlaji wa huduma ya fedha na mpango huo umetoa maelekezo ya utoaji elimu ya fedha nchini.
 
Bw. Kibakaya aliongeza kuwa mpango huo wa miaka 10 ambao utekelezaji wake umeanza mwaka 2020/21, Wizara imejiwekea malengo hadi kufikia mwaka 2025 kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wamepata uelewa wa masuala ya fedha na waweze kuzitumia vizuri fursa zinazopatikana katika sekta ya fedha nchini.
 
Aidha Bw. Kibakaya alisema kupitia mafunzo yaliyotolewa kwa wananchi wa Morogoro yatasaidia kwa watoa huduma ndogo za fedha na wanufaika wa huduma hizo kufuata sheria za huduma ndogo za fedha na kanunuzi zake kama zinavyoelekeza.
 
Serikali iliamua kutoa elimu ya fedha kwa wananchi baada ya kugundua kuwa kuna kundi kubwa la watanzania ambao hawafaidiki na huduma za fedha na hivyo kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi na hatimaye kuchangia katika kukuza pato la Taifa.
Share To:

Post A Comment: