Waziri wa Madini Anthony Mavunde ataka fedha  zinazotolewa kama sehemu ya gawio la mrabaha kutoka katika mgodi zitumike katika miradi iliyoibuliwa na wananchi katika sehemu husika kwa ajili ya kuendeleza mipango ya maendeleo kwa wananchi .

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde wilayani Tarime  mkoani Mara wakati wa  hafla fupi ya kukabidhi mfano wa hundi tano za malipo ya mirabaha kwa vijiji vitano kutoka katika mgodi wa dhahabu wa North Mara.

Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Serikali kupitia mpango wa CSR  inatambua mchango wa migodi kwa jamii, hivyo fedha hizi zinazotolewa katika vijiji vitano  zikatumike kikamilifu katika maeneo husika ili kuleta uhalisia na  kuonesha umuhimu wa uwekezaji uliopo ndani ya sekta ya madini nchini.

Akielezea kuhusu ushirikishwaji wa Vijana , Wakina mama na Wazee katika sekta ya madini eneo la Nyamongo , Waziri Mavunde ameigiza Tume ya Madini kupitia Ofisi ya Afisa Madini Mkazi  Tarime kushirikiana na Ofisi ya Mkoa wa Mara kutenga maeneo maalum yatakayofanyiwa utafiti na kugawiwa kwa makundi hayo kwa ajili kufanya uchimbaji wenye tija.

Akifafanua kuhusu mpango wa  utekelezaji wa Maudhui ya Ndani (Local Content), Waziri Mavunde amesema , Wizara ya Madini itashirikiana na Wizara ya Kilimo kwenye mradi wa uchimbaji visima vya maji kuchimba visima katika eneo la Nyamongo ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa maji kwa kilimo cha mbogamboga kama walivyoanza.

Awali ,  akiwasilisha taarifa kuhusu maendeleo ya utoaji wa gawio la mrabaha wa asilimia moja kwa vijiji vitano Meneja Mkuu wa Mgodi wa NorthMara Ndg.Apolinary Lyambiko amesema kampuni ya Twiga katika Robo ya Pili ya mwaka 2024 imetoa mrabaha wa zaidi ya shilingi bilioni 1.1 katika vijiji vitano ikifanya jumla ya Shilingi Bilioni 2.2 kutolewa kwa vipindi vya robo ya kwanza na ya pili ya miaka.

Lyambiko amevitaja vijiji hivyo nufaika kuwa ni pamoja na Kerende,Kewanja,Nyamwaga,Nyangoto na Genkuru.North Mara Gold Mine Limited imeendelea kutoa gawio la Mrabaha kwa vijiji 5 ambavyo vilikuwa vikimili maeneo yenye leseni za uchimbaji (PML) wakati mgodi unaanzishwa na Kampuni ya Afrika  Mashariki Gold Mines Limited (Sasa North Mara Gold Mine Limited) mnamo tarehe 27 April 1996

Lyambiko ameongeza kuwa, kwa kipindi  cha miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2024 kiasi cha bilioni 69 kimelipwa kwa Serikali ikiwa ni malipo mbalimbali yanayotokana na  Mgodi.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Masache Kasaka ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya madini  hususani kwenye uwazi katika utoaji wa mirabaha.

Nae, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja. Edward Gowele ameipongeza Serikali kupitia wizara ya madini kwa kazi nzuri inayofanya katika kushirikisha jamii kwenye miradi ya kitaifa ikiwa ni mipango na mikakati ya kuwanufaisha kwenye rasilimali zinazowazunguka katika maeneo yao na kuhaidi kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro yote iliyopo katika wilaya ya Tarime.

Akizungumza kwa niaba ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Lemi Mkapa ameishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wa Nyamongo kwa kuweka mpango wa wazi katika utoaji wa mrabaha ambapo kupitia fedha hizo jamii itaibua miradi ya kijamii na kutatua changamoto zilizopo.

Share To:

Post A Comment: