Msimu wa pili wa Tamasha la Twenzetu Tukacharu Rau Forest – Mtoko Nyika 2024 umezinduliwa rasmi ambapo washiriki zaidi ya 1000 kutoka mataifa mbalimbali watashiriki tukio hilo litakalofanyika katika Msitu wa Rau mjini Moshi.
Tukio Tukacharu Rau forest ikiwa na maana ya Twenzetu tukatembee/tukakimbie Rau Forest linalenga kuhamasisha shughuli za utalii na kutangaza utalii wa ndani, kwenye msitu huo, litaenda sambamba na mbio za baiskeli na utalii wa asili 'kutembea peku' ndani ya msitu.
Akizindua msimu wa pili wa Tukacharu Rau Forest, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema shughuli hiyo itahitimishwa Agosti 24 na 25 mwaka huu ambapo katika siku hizo watalii watapata fursa ya kuona vivutio mbalimbali ikiwemo panya wenye masikio kama ya Tembo, Mbega mwepe na mvule mkubwa Afrika.
"Tutaanza leo shughuli yetu ya Tukacharu, na lengo letu mahususi ni kuutangaza utalii wa ndani na kwa kuwa msitu huu uko mjini Moshi na kwa jinsi ulivyohifadhiwa ukiingia huku ndani mandhari yake huwezi kuamini kama upo mjini, na ndani ya msitu huu tuna maeneo ya pikiniki, na nyama choma na kupata vinywaji baridi na moto pamoja na kuona vivutio vingi ambavyo watakaofika watavishuhudia na kufurahia "amesema Sumaye.
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Moshi, Godson Ulomi amesema Tukacharu mwaka huu imeboreshwa zaidi ikilinganishwa na mwaka jana ambapo kutakuwa na mashindano ya mbio za baiskeli Kilometa 75, kukimbia kilometa tano na 21 pamoja na matembezi ndani ya msitu huo.
"Tukacharu awamu ya kwanza ilifanyika mwaka jana na hatua hiyo iliongeza idadi ya watalii katika msitu wa Rau na kwa mwaka huu tumeboresha zaidi ambapo mashindano ya baiskeli, kukimbia na matembezi ndani ya msitu"amesema Ulomi
Ameongeza kuwa "Usiku wa Agosti 24 kuamkia Agosti 25 ambayo ni kilele, kutakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo ngoma za asili, vyakula vya asili, lakini kuna watakaopiga kambi na michezo mbalimbali ya asili ambayo itakuwa sehemu ya burudani".
Zayana Mrisho, ambaye ni mratibu wa tamasha hilo amesema watakuwepo washiriki zaidi ya 1,000 ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuwaalika wadau mbalimbali ambao watahitaji kutangaza biashara zao kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo.
"Matembezi ya asili ikiwemo kutembea peku kiingilio itakuwa ni Sh 17,000, kukimbia kilometa 5, 21, na mashindano ya baiskeli watalipa Sh35,000, lakini watakaopiga kambi watalipia Sh43,000".
Post A Comment: