Timu ya mpira wa miguu ya Wizara ya Ardhi,  Nyumba na Maendeleo ya Makazi imechuana vikali na wenzao wa Ofisi ya Rais Ikulu ikiwa ni maandalizi ya michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayotarajiwa kuanza Septemba 18, 2024 mkoani Morogoro.

Mgeni Rasmi katika mchezo huo Bw. Simbani Liganga, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu Wizarani hapo amesisitiza wachezaji na watumishi kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha afya zao hatua itakayosaidia kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Mchezo huo umefanyika Agosti 23, 2024 katika viwanja vya Shule ya sekondari ya St. John Merline iliyopo Miyuji jijini Dodoma.

Rekodi inaonesha timu za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika michezo ya mpira wa miguu, netiboli, riadha, mchezo wa kamba wanaume na wanawake, mchezo wa bao, karata na mbio za baiskeli ni miongoni mwa timu ambazo hutoa upinzani mkali kwa timu wanazokutana nazo katika michuano ya SHIMIWI.

Viongozi wa Kitaifa mara kwa mara wamekuwa wakihimiza watanzania wakiwemo watumishi wa umma kufanya mazoezi ili kuwa na afya njema inayowawezesha kutoa huduma bora kwa weledi zaidi. 

Hiki ni kipindi cha maandalizi kwa timu mbalimbali katika wizara na Idara za Serikali kuelekea Michuano ya SHIMIWI ambayo hushirikisha watumishi wa umma takribani 3000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Share To:

Post A Comment: