MENEJA wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),Mkadiriaji Majenzi, Qs. Emanuel Wambura,akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda TBA wakati wa Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane, yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni,jijini Dodoma.

AFISA Masoko TBA Kristolearachel Msengi akitoa elimu kwa wananchi waliofika kwenye banda la TBA wakati wa Maonesho ya Kitaifa ya Nanenane, yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni,jijini Dodoma.


Na.Mwandishi Wetu-DODOMA


Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetumia Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane, yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya ujenzi.

Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, Mkadiriaji Majenzi, Qs. Emanuel Wambura, amesema kuwa TBA inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu miradi ya ujenzi inayotekelezwa na wakala huo, hususan katika sekta ya kilimo.

Aidha, Wambura ameongeza kuwa TBA inaendelea kushirikiana na wakulima kwa kuwashauri juu ya mbinu bora za ujenzi wa nyumba za makazi na kuboresha miundombinu ya biashara ya mazao ya kilimo.

"Tunaendelea kuwashauri wakulima kuhakikisha wanajenga nyumba zao kwa viwango vya juu, sambamba na kuboresha miundombinu inayochangia ufanisi katika biashara ya mazao ya kilimo," alieleza Wambura.

Pia, TBA imesimamia mradi mkubwa wa ujenzi wa vihenge na maghala ya kuhifadhia chakula katika mikoa takribani nane nchini, ambapo mikoa mitatu tayari imemaliza utekelezaji wa mradi huo.

"Mradi huu ni wa muhimu sana kwa wakulima kwani unawasaidia kuhifadhi mazao kama mahindi, ambayo yanapata thamani zaidi kabla ya kupelekwa sokoni," aliongeza.

Sambamba na miradi ya kilimo, TBA pia imetekeleza miradi katika sekta ya mifugo kwa kubuni na kujenga soko la mnada wa mifugo katika Mkoa wa Geita.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: