Tanzania inatarajiwa kuwa miongoni mwa nchi tano za Afrika zitakazonufaika na ujenzi wa mradi mkubwa wa Hospitali itakayokuwa na viwango vya dunia vya utoaji huduma za matibabu (African Medical Center of Excellence (AMCE), kupitia mradi unaotekelezwa na African Export-Import Bank (Afreximbank) kwa kushirikiana na Hospitali ya Chuo Kikuu cha King, iliyoko London nchini Uingereza.
Hayo yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Umahili cha Kimatibabu, Abuja, Bw. Brian Deaver, wakati Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alipoongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea ujenzi wa mradi wa aina hiyo, nje kidogo ya mji wa Abuja, nchini Nigeria.
Bw. Deaver alieleza kuwa Hospitali hiyo itakayokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 500 kwa wakati mmoja, itatumia teknolojia ya kisasa ambayo haijawahi kutumika katika Bara la Afrika kwa ajili ya kutibu magonjwa ya kansa ya damu na sickle cell.
Alifafanua kuwa Hospitali hiyo pamoja na hospitali nyingine zitakazojengwa nchini Ghana, Kenya na Tanzania, zitatoa huduma mtambuka ikiwemo uchunguzi, matibabu, tiba kwa anjia ya nyuklia, upasuaji, huduma baada ya upasuaji na huduma nyingine zinazojulikana kitaalam kama oncology, haematology na magonjwa ya moyo.
“Tunapotekeleza mradi huu tunalenga kutoa huduma bora za afya, kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya, kufanya utafiti, kutoa ajira, kudhibiti mahitaji ya matumizi ya fedha za kigeni hususan dola na kukuza utalii wa kimatibabu kwa nchi za Afrika” aliongeza Bw. Deaver
Wakizungumza baada ya kutembelea mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 260, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Elmaanry Mwamba, walisema kuwa mradi huo wa mfano si tu kwamba utasaidia huduma za kimatibabu kwa wananchi, bali pia itakuwa sehemu ya utalii wa kimatibabu kwa watu kutembelea na kupata huduma hizo kutoka nje ya Tanzania.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Bi. Judica Nagunwa, alisema kuwa jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya uchumi na matibabu, umelenga kuimarisha afya za watanzania na kwamba ubalozi wake utatumia kila fursa kuhakikisha kuwa mradi huo unatekelezwa kwa manufaa ya watanzania.
Afreximbank ni Taasisi ya fedha ya kimajumui ya kimataifa (Pan-African multilateral financial institution) yenye majukumu ya kutoa fedha na kuendeleza biashara kwenye nchi za Afrika.
Dkt. Nchemba, ameongoza ujumbe wa Tanzaniaakiwa na Ujumbe wa Tanzania, akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango-Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, wanashiriki Mikutano ya Nchi za Afrika (African Caucus Meetings), uliowashirikisha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka nchi wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Post A Comment: