Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imeweka mipango na mikakati ya kuhakikisha watoto wanapata malezi bora yanayolenga kukuza ustawi wao.
Mhe. Ridhiwani amebainisha hayo leo Agosti 16, 2024 wakati wa makabidhiano ya vyerehani vya mafunzo ya vitendo kwa ajili ya watoto wanaolelewa katika Makao ya Taifa ya kulelea Watoto Kikombo, Jijini Dodoma.
Aidha, amesema kuwa dhamira ya serikali inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuboresha ustawi na malezi ya watoto nchini ambao ni vijana na wataalamu wa baadae.
Vile vile, Mhe. Ridhiwani ametaka Wizara, Walezi na Idara zinazohusika kuwashirikisha wadau wa maendeleo ya Jamii ili kuhakikisha vituo vya kulelea watoto vinafanana katika kutoa huduma bora.
Awali akizungumza, Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameitaka jamii kuendelea kushirikiana na serikali katika huduma za ulinzi na usalama wa watoto zinazotolewa katika kituo hicho kwa maslahi mapana ya Taifa.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Zuhura Yunus amesem ugawaji wa vyerehani hivyo ni hatua nzuri kwa WCF kutambua umuhimu wa kundi hilo kupata ujuzi.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema vyerehani ambavyo vimekabidhiwa katika kituo hicho ni utekelezaji wa sera ya kurejesha kwa jamii na miongoni mwa walengwa ni makundi maalum wakiwemo watoto hao.
Post A Comment: