SERIKALI imezindua Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 toleo la 2024, ambayo inakwenda kutatua changamoto mbalimbali za vijana nchini.


Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center jijini Dodoma.

Akizungumza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Ridiwani Kikwete amesema Serikali katika kuhakikisha masuala ya maendeleo ya vijana yanapatiwa mwongozo na mwelekeo imekwisha kamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 na toleo la mwaka 2024.

Aidha, Mhe. Ridhiwani amesema Sera hiyo inaendana na mabadiliko mbalimbali ya jamii, kiuchumi, kisiasa na kiteknolojia.

"Serikali inaelewa kuwa mchango wa vijana katika maendeleo ya kidijitali ni muhimu sana kwa vile vijana ni wabunifu, wanajua kutumia teknolojia na wanauwezo wa kuleta mabadiliko makubwa katika jamii zetu," amesema Mhe.Ridhiwan

Amesema, ujio wa sera hiyo ya vijana kutachagiza uudwaji wa baraza la taifa la vijana ikiashiria azma ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto zinazo wakabili vijana kwa kuzipatiwa majibu.

Kwa upande mwengine, Waziri Ridhiwani amewataka watendaji wa ofisi yake kuendana na mabadiliko ya sasa katika kuwahudumia wananchi.

Naye, Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Mary Maganga, amesema katika kuadhimisha siku ya vijana, wameendesha kongamano la siku mbili lililokutanisha vijana zaidi ya 3,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

"Katika kongamano hilo, vijana wamepata fursa ya kutoa maoni juu ya Dira ya Maendeleo ya 2050, fursa za kidigitali, vijana na uchumi, afya ya akili na saikolojia ya vijana, ajira na uwezeshaji." amesema Maganga

Naye Mwakilishi wa Vijana, Charles Ruben ametoa pongezi kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuwasaidia na kuwainua vijana.




Share To:

Post A Comment: