Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Cuthbeth Sendiga amewahimiza wafugaji na wakulima wa mikoa ya kanda ya kaskazini ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro, kuwekeza kwenye teknolojia na kilimo na ufugaji wa kisasa, ili kuondokana na migogoro ya ardhi kati ya Wakulima na Wafugaji.
Mhe. Sendiga ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Agosti 08, 2024 wakati akifunga maonesho ya 30 ya kilimo na mifugo maarufu kama Nanenane yaliyohitimishwa kwenye viwanja vya Themi Njiro Wilayani Arusha na kuhusisha watazamaji 49, 725 na makundi 15 yaliyokuwa na waoneshaji takribani 402.
"Wananchi wanaongezeka, shughuli za kilimo zinaongezeka, mifugo inaongezeka lakini ardhi haiongezeki kwahiyo ni lazima tuende kwenye teknolojia ya kisasa ili kuendana na eneo la ardhi tulilonalo.Tufike sehemu tukubali kufuga mifugo michache kwa afya bila ya msongo wa mawazo.', ameongeza Mhe. Sendiga.
Katika hatua nyingine pia Mhe. Sendiga ametoa wito kwa Halmashauri zote 21 za Mikoa ya kaskazini wakiongozwa na Makatibu tawala wa mikoa wametakiwa kusimamia kikamilifu asilimia 20 za Halmashauri zinazotakiwa kutengwa kwaajili ya uvuvi na kilimo kama ilivyo maelekezo ya serikali kama sehemu ya kusisimua uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Aidha Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Manyara amewataka watazamaji wa maonesho hayo kwenda kutumia vyema elimu za kilimo na ufugaji walizozipata kwenye maonesho hayo pamoja na kuwajengea watoto utamaduni wa kupenda kilimo kwa kuwaanzishia bustani ndogondogo za mbogamboga kwenye maeneo yao.
Mhe. Sendiga pia ametumia sehemu ya hotuba yake kuhamasisha wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la mpigakura pamoja na kujitokeza kupigakura na kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadae mwaka huu.
Kaulimbiu ya maonesho ya nanenane kwa mwaka huu 2024 inasema "Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi."
Post A Comment: