Na Denis Chambi, Tanga.
FAMILIA ya Marehemu Bakari Kidawa kutoka wilaya ya Tanga Mkoani hapa wametua kilio chao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu wakimuomba kuingilia kati mgogoro wao mashamba kati yao na uongozi wa Halmashauri ya jiji la Tanga ambao kwa umedumu mrefu licha ya kufuatilia kwa zaidi ya miaka 10 lakini bado hawajapata mwarobaini.
Wakizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Jijini hapa watoto hao walieleza kuwa wamelazimika kumuomba Rais Dkt Samia kuingilia kati baada ya kukosa msaada kutoka kwa mamlaka mbalimbali kuanzia ofisi ya ardhi , mipango miji ambazo zimeshindwa kuwapatia haki yao licha ya kuwepo na vielelezo vinavyoonyesha uhalali wao wa kumiliki mashamba hayo yenye ukubwa zaidi ya hekali 10 .
Akizungumza mmoja wa wanafamia hao Koja Kidawa alisema kwamba mgogoro huo ulianza mwaka 1,996 hata kabla ya marehemu baba yao hajafariki ambapo Kamishna Mkuu wa Ardhi aliziagiza mamlaka za Tanga kuwasikiliza na kuona namna watakavyoweza kuwasaidia kuutatua.
Kwa mujibu wa Koja Kidawa alisema kwamba baadhi ya mashamba ya marehemu baba yako yalichukuliwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Mkoa wa Tanga na baadhi ya wafanyakazi wa Serikali bila kuwa na ridhaa ya marehemu baba yao.
Alisema hata hivyo Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Mkoa wa Tanga lilikanusha kutwaa maeneo yao bali walikiri kugawiwa maeneo hayo na Ofisi ya Mipango Miji ya jiji la Tanga baada ya kuomba maeneo hayo ambayo yanapakana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Aidha alisema baada ya kuona wanapigwa danadana na mamlaka za Serikali mkoani Tanga ambazo ni Ofisi ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Jiji la Tanga pamoja na Mkurugenzi wa Jiji hilo Dkt Frederick Sagamiko na hivyo kulazimika kwenda Jijini Dodoma kuona na Kamishna Mkuu wa Ardhi ambaye aliwaandikia barua mamlaka za Tanga kuwahimiza kulitatua suala hilo haraka iwezekanavyo.
Alisema hata hivyo viongozi hao wa Tanga akiwemo Afisa Mipango Miji na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga hawajaonyesha dalili za kutaka kuwasaidia ili wapate haki yao ambayo wanaidai na hivyo kulazimika kufika kwenye vyombo vya habari ili kumuomba Rais Dkt Samia Suluhu kuona namna ya kuwasaidia kutokana na kukosa fedha za kufuatilia suala hilo.
“Katika mgogoro huu tulilazimika kwenda kuonana na viongozi wa mkoa wa Tanga akiwemo Afisa Mipango Miji, Mkurugenzi wa Jiji na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa lakini hawakuonyesha dalili zozote za kutusaidia ndio maana tukaona ni muhimu tukuombe Mhe Rais Dkt Samia Suluhu utusaidia suala hili “Alisem
Kwa upande wake Kidawa Bakari Kidawa alidai kwamba katika eneo lengine la kwao Mipango Miji ililigawa kwa Mmiliki wa Shule ya Prince and Princes anayetambulika kwa jina la CN Mushi.
Kidawa alisema kwamba familia hiyo ina matumaini makubwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwamba suala lao litashughulikiwa mapema na kuweza kupata haki yao ya msingi
“Tunamjua Rais Samia Suluhu ni mama mwenye huruma na sisi kama wanawe tunaamini ataingilia kati suala hili ili tuweze kupewa haki yetu “Alisema Kidawa Bakari Kidawa ambaye ni mtoto wa pili wa marehemu.
Hata hivyo jitihada za waandishi wa habari kutaka kupata majibu kuhusiana na sakata hilo kwa mamlaka husika ziligonga mwamba baada ya wahusika akiwemo Ofisa Mipango Miji wa Jiji la Tanga Mussa ambaye alidai hawezi kuzungumzia suala hilo mpaka apate kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Jijini pamoja na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Tanga .
Post A Comment: