Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ametoa rai kwa Mamlaka za Serikali pamoja na wawekezaji kutoka Sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika Sheria ya Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kupata faida na kuipunguzia Serikali mzigo wa kibajeti.  

Mhe. Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo Mjini Dodoma, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya, kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, sura Na. 410, Sheria ya Ubia kati ya sekta ya Umma na Binafsi, Sura Na. 103 na mafunzo ya matumizi ya takwimu zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma, uliopo Mji wa Serikali Mtumba. 

Aliwahimiza Maafisa Masuuli wote kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Hazina namba 7 wa mwaka 2020/21 unaotoa maelekezo na mwongozo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa PPP.

Alisema kuwa Sheria ya PPP Sura 103 imefanyiwa marekebisho kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, Sheria hiyo inaruhusu wawekezaji katika miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyokuwa vya kikodi, sawa na wale wanaopata vivutio chini ya Sheria ya Uwekezaji Tanzania, Sura ya 38. 

“Sheria ya PPP inaruhusu taasisi za umma kununua mbia anayekidhi vigezo moja kwa moja kwa miradi isiyohitaji ushindani ili kupunguza muda wa hatua za ununuzi na pia imetoa fursa kwa wawekezaji wa kigeni kushirikisha wazawa katika miradi ya PPP ili kuwawezesha kiuchumi na kuendeleza wataalamu wa ndani”, alisema Dkt. Nchemba.

Akizungumzia suala la matumizi sahihi ya Takwimu Dkt. Nchemba alisema kuwa maendeleo ya Taifa lolote ulimwenguni yanatokana na matumizi sahihi ya takwimu zilizozalishwa na vyombo vyenye jukumu hilo katika kupanga mikakati mbalimbali ya maendeleo.  

Alisema kuwa utekelezwaji wa mipango yote ya mendeleo nchini Tanzania umekuwa ukifanywa kwa kuzingatia takwimu zilizoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ambayo ilianzishwa kwa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 ambayo imeipa mamlaka ya kuandaa na kuchapisha takwimu mbalimbali zinazohitajika kwa matumizi ya kimaendeleo ikiwemo kiuchumi, kijamii na kisiasa.  

Dkt. Nchemba alisema pamoja na kuwepo kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu inayofanya kazi nzuri ya kutoa takwimu mbalimbali, bado matumizi ya takwimu hizo katika upangaji na utekelezaji wa mipango hauridhishi, kwa kuwa mara kadhaa imetiliwa mashaka kama ilitumia takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu. 

“Mipango yenye mashaka inatupotezea muda lakini pia imekuwa ni chanzo cha kutofanikishwa kwa malengo mbalimbali hususani malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi, natoa rai kwa taasisi zote za umma hapa nchini kuhakikisha zinazingatia na kuongeza matumizi ya takwimu zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu katika kuandaa mipango yote muhimu kwa kadri inavyowezekana”, alisisitiza Dkt. Nchemba.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, alisema kuwa katika historia ya nchi ya Tanzania hakuna kipindi ambacho Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa zimetekeleza miradi mingi kama kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema bajeti kubwa ya Serikali inaenda TAMISEMI na kwa kiasi kikubwa inatumika kwenye ununuzi katika utekelezaji wa miradi lakini pia shughili mbalimbali za kiofisi.

Alisema kuwa katika taarifa nyingi za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kumekuwa na changamoto kubwa kwenye eneo la ununuzi, hivyo mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa watendaji walioshiriki ili kuweza kutekeleza shughuli zao hususani za ununuzi lakini kutumia takwimu sahihi kupanga mipango ya maendeleo

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa walioshiriki Mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Martin Shigella, alisema kuwa wanapopata majukwaa ya mafunzo kama hayo yanasaidia kujua jambo gani la kufanya ili kusukuma jambo ambalo limekwama katika mkoa husika.

Aidha alimshukuru Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Nchemba kwa kuwaalika na wapo tayari kufanyia kazi yale yote yatakayowasilishwa kupitia mada mbalimbali katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Mkutano huo umewashirikisha Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya.

Share To:

Post A Comment: