NAIBU Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa amewataka viongozi wa milla maarufu kwa jina la Laigwanani na viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi{CCM} ngazi ya Kitongoji,Kijiji na Kata kuwahimiza akina mama wajawazito wa jamii  ya kifugaji ya kimasai kuhakikisha wanakwenda kujifungua katika vituo vya afya na sio nyumbani ili kuepusha vifo vilisivyo vya lazima.

Dkt Kiruswa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Longido alisema hayo katika kituo cha afya cha Ngarenaibor wilayani Longido wakati akikabidhi vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5 ambavyo vinakwenda kuboresha utoaji wa huduma za Afya ndani ya jimbo hilo na kwenda kuwawezesha wananchi wengi kuwafikia kupata huduma muhimu ya afya.

Alisema serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inajitahidi kutafuta mamilioni ya fedha nje kwa ajili ya wananchi wote wan chi hii kupata tiba ya uhakika na akina mama wajawazito kupata vifaa tiba vya kujifungulia lakini inasikitisha kuona baadhi ya akina mama wa Jamii ya Kimasai wanajifungulia nyumbani katika mazingira ambayo sio rafiki

Naibu Waziri huyo alisema hilo haliwezekana na kuwaagiza viongozi wa Milla na serikali wa ngazi zote kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii hiyo kuacha kujifungulia nyumbani na kwenda katika vituo vya afya ili kupata huduma safi na salama.

KITUO CHA AFYA ENGARENAIBOR KIMEANZA KUTOA HUDUMA YA UPASUAJI

Hivi vifaa mvitunze na muhakikishe vinadumu na vinakwenda kutoa huduma kwa wananchi,ila muendelee kuwasisitiza wananchi wa jamii yetu ya Kimasai kuja kupata huduma ya kujifungulia katika vituo hivi vilivyojengwa na Rais Samia Suluhu Hassan  ili kuendelea kuhakikisha wanapata uzazi salama na kuepuka vifo visivyo vya lazima" Alisema

Sambamba na hilo Dkt. Kiruswa alisema ataendelea kuhakikisha anatatua mapungufu yote yaliyopo katika sekta ya Afya katika Jimbo la Longido likiwemo la upungufu wa watumishi ili kuweza kuziba mapungufu yote yaliyomo katika Vituo vyote vya Afya katika jimbo hilo lenye wakazi wengi wa jamii ya kifugaji.

Kwa upande wake diwani wa viti maalum jimbo la Longido Mensiana Bendera  ameishukuru serikali kwa kuendelea kuwapigania wanawake kwani vifaa tiba hivyo vitakwenda kuwasaidia wanawake wa jamii ya kimasai.

Alisema jukumu walilonalo ni kuhakikisha akina mama wa jamii ya kimasai inakwenda kujifungulia katika vituo vya afya ila ombi kwa serikali ni kwa watumishi kupata nyumba za uhakika ili waweze kuifanya kazi hiyo kwa umakini kuliko hivi sasa wanatoka mbali na kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido,Nassoro Shemzigwa amemuhakikishia Mbunge wa jimbo hilo kuwa majengo yote ambayo hayajakamilika pamoja na mapungufu madogo yaliyoko katika vituo vya afya katika wilaya hiyo watakwenda kushirikiana na wananchi wa kata zote 18 sambamba na Baraza la Madiwani ili kuhakikisha kila kituo cha afya kinakwenda kufanya kazi kama ambavyo ilikusudiwa na serikali ya Rais samia Suluhu Hassan.

Alisema changamoto za kukosekana kwa nyumba za watumishi wa afya katika wilaya ya Longido changamoto hiyo nayo itatafutiwa dawa ili kila mtumnishi aishi katika nyumba ya serikali ili aweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.





Share To:

Post A Comment: