Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyoba amesema Kituo cha kupoozea umeme cha Ifakara ni kituo bora na mkombozi wa Wilaya za Ulanga na kilombero pamoja na vijiji vyake vyote.
Ameyasema hayo alipotembelewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) leo tarehe 03 Agosti 2024 wilayani Kilombero walipokuwa wakijadili ziara ya Mhe.Dkt .Samia Suluhu Hassan Mkoani Morogoro ambapo atafanya ziara siku ya jumapili tarehe 4 Agosti,2024 katika kituo cha kupozea umeme kilichojengwa na REA kwa ufadhili wa umoja wa Ulaya pamoja na Serikali ya Tanzania.
"Kituo hiki cha kupozea umeme ni cha kisasa na tangu kianze kufanya kazi kimeendelea kuchochea ukuaji wa uchumi katika Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi," amesema Mhe. Kyoba.
Amefafanua kuwa umeme wa uhakika unahitajika katika uendeshaji viwanda vya uchimbaji wa madini aina ya graphite katika wilaya ya Ulanga na uongezaji thamani mazao ya chakula hususan mahindi na mpunga.
Alipongeza REA kwa kupunguza kero za upatikanaji umeme katika sekta ya afya wilayani Kilombero hususani katika hospitali ya St.Francis na Good Samaritan mjini Ifakara.
"Wilaya ya Kilombero ni Wilaya ya Uhifadhi hivyo kituo hiki cha kupozea umeme kimepunguza kasi ya ukataji miti hovyo na hivyo kupungua kwa kiasi kikubwa cha uharibifu wa misitu," amesema Mhe.Kyoba
Aidha, ameisisitiza REA kuhakikisha inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na masuala mazima ya nishatisafi ya kupikia pamoja na ugawaji wa mitungii ya gesi kwa wananchi wa Wilaya ya kilombero na vijiji vyake kwani.
"Kilombero imefunguka matumizi ya gesi ya kupikia yataongezeka ikiwemo matumizi mazima ya nishati mbadala na majiko ya banifu, tuendelee kuhamasisha wananchi," amesisitiza.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha.Hassan Said amesema miradi ya REA imetawanyika nchi nzima hivyo nia kubwa ya Wakala ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini kufikia Desemba 2024 vinakuwa na umeme.
"Maisha ya watanzania waishio vijijini watatumia umeme huu sio kuwashia taa tu bali kubadilisha maisha yao kiuchumi kwa kuwa na shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato," amesema Mhandisi Said.
Wakala wa Nishati Vijijini REA,ulianzishwa kwa malengo kuwezesha upatikanaji wa nishatisafi vijijini.
Post A Comment: